NAHODHA wa Klabu ya Simba, John Bocco amesema kuwa nyota wa kikosi hicho wameapa kuwa hawatakubali kufungwa tena na Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation utakaopigwa Julai 12 jijini Dar.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Bocco alisema wamefurahi kutinga katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na kuahidi kuwa lazima washinde mchezo huo kwa kuwa wanautaka ubingwa wa pili msimu huu.“Tunafurahi kwa kupata nafasi ya kufika katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii, tunajua mbele yetu kuna mchezo mgumu dhidi ya Yanga ambao utaamua ni nani atapata nafasi ya kucheza fainali na labda kuwa bingwa wa mashindano haya.

 

“Katika michezo miwili iliyopita ya ligi kuu tuliyokutana msimu huu wenzetu waliweza kupata pointi nne na kutuachia pointi moja tu, hivyo kwa kuwa tuna malengo ya kutwaa ubingwa huu tutahakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huu na hatutakubali kupoteza mchezo kwa mara ya pili mfululizo,” alisema Bocco.