JESHI la Polisi  Kanda Maalum  Dar es Salaam limewaua majambazi watatu na kukamata silaha mbili aina ya Short Gun Pump Action na Bastola aina ya Browning.

Mnamo tarehe 26.07.2020 majira ya saa mbili usiku  Jeshi la Polisi Kanda Maalum lilipata taarifa kuwa huko maeneo ya Mbagala Chamanzi kuna gari lenye namba T 855 ATE aina ya Nissan X-Trail likiwa na watu wanne  wanaosadikiwa  kuwa ni majambazi wakiwa katika harakati za kufanya uhalifu.

Baada ya kupata taarifa hizo kikosi kazi cha kupambana na ujambazi kiliweka   mtego  katika eneo hilo na baada  majambazi hao kuhisi wanafuatiliwa na Polisi ghafla   walianza kupiga risasi hovyo kwa hofu na ndipo askari wakaamua kujibu mapigo kwa kulishambulia gari la majambazi hao  na kufanikiwa  kuwaua papo hapo majambazi watatu na jambazi mmoja akafanikiwa kukimbia.

Askari walifanya upekuzi ndani ya gari la majambazi hao na kumkuta jambazi mmoja akiwa amevalia mavazi ya Jeshi la Polisi aina ya kombati za kijani (JUNGLE GREEN) na kofia aina ya bareti nyeusi ya Jeshi la Polisi, redio Call, Pingu, namba za gari T 832 DCW ambazo ndiyo namba halisi za usajili wa gari hilo na silaha mbili aina ya Short gun Pump Action ikiwa na risasi nne ndani ya magazine iliyofutwa namba na Bastola aina ya Browning iliyofutwa namba ikiwa na risasi nne ndani ya Magazine.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa majambazi hao walifanya matukio ya uhalifu Mkoa wa Pwani Wilaya ya Mkuranga maeneo ya Vikindu na Kisemvule ambapo mnamo tarehe 25/07/2020  majira ya saa mbili usiku majambazi hao walimteka na  kumpora mfanyabiashara wa UWAKALA wa Benki na Mitandao ya simu aliyefahamika kwa jina la  SALEHE  MASOUD kiasi cha Tsh 19,600,000/=  .

POLISI KANDA MAALUM KUIMARISHA ULINZI SIKUKUU YA EID EL-HAJJI.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum kwa  kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi cha sikukuu ya Eid El-Hajji inayotarajiwa kuadhimishwa tarehe 31/07/2020.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawaasa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kusherehekea sikukuu  kwa amani na utulivu na kujiepusha  na vitendo vya uvunjifu wa sheria kwani tumejipanga kuimarisha doria maeneo yote muhimu zikiwemo nyumba za Ibada, fukwe za bahari na tunawatadharisha watembea kwa miguu na madereva wa vyombo vya moto kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani.

Aidha Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawaomba Wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu  kwani jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila Mtanzania.
 
SACP- LAZARO B. MAMBOSASA,
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.
30/07/2020.