Maafisa nchini Indonesia wameapa kumaliza utamaduni wenye utata wa kutekeka nyara wanawake ili kuwa bibi harusi katika maeneo ya vijijini kisiwa cha Sumba, baada ya video za wanawake kutekwa nyara zilizosambaa mitandaoni kusababisha mjadala mkali kuhusu utamaduni huo.
Citra alifikiria tu kwamba ni mkutano wa wafanyakazi. Wanaume wawili waliodai kuwa maafisa wa eneo walisema wanataka kupitia bajeti ya mradi aliokuwa anaendesha katika shirika moja la kutoa msaada.
Mshichana wa, 28, alikuwa na wasiwasi kuhusu kile kinachoendelea lakini akaendelea kuwa makini na kazi yake anayofanya, na kuondoa wasiwasi huo.
Saa moja baadae, wanaume hao walipendekeza kwamba mkutano huo uendelee katika eneo tofauti na kumuomba apande kwenye gari lao.
Lakini baada ya mwanamke huyo kusisitiza kwamba atatumia pikipiki yake, ghafla kundi la wanaume kikamkamata kwa nguvu ghafla.
“Nilikuwa ninarusharusha miguu na kupiga kelele, walipokuwa wananilazimisha kuingia kwenye gari. Sikuwa na usaidizi wowote. Ndani ya gari kulikuwa na watu wengine wawili walionishika,” anasema. “Moja kwa moja nikafamu nini kinachoendelea.”
Alikamatwa ili akaolewe.

Kutekwa kunyara mwanamke ili akaozwe au kawin tangkap kama inavyofahamika, ni utamaduni uliozua utata ambao unaendelea eneo la Sumba. Wanawake huchukuliwa kwa lazima na wanafamilia au marafiki wa mwanaume anayetaka kumuoa.
Licha ya uwepo wa wito wa muda mrefu na makundi ya haki za wanawake, bado utamaduni huo unaendelea kutekelezwa katika baadhi ya sehemu za eneo la Sumba, eneo la vijijini mwa Indonesia kisiwa cha mashariki mwa Bali.
Lakini baada ya wanawake wawili kutekwa nyara na tukio hilo kurekodiwa kwenye video na kusambazwa katika mitandao ya kijamii, serikali kuu sasa imetoa wito wa utamaduni huo kukomeshwa.
‘Nilihisi kana kwamba ninakufa’
Ndani ya gari, Citra alifanikiwa kumtumia mchumba wake na wazazi wake ujumbe kabla ya kufika kwenye nyumba ya kuendesha utamaduni huo. Kisha akagundua kwamba familia iliyomteka nyara, ni jamaa wake wa mbali upande wa baba yake.
“Kulikuwa na watu wengi wanaonisubiri nilikokuwa ninapelekwa. Walisikika kama waliopata ushindi wakati ninawasili na wakaanza utamaduni wao.”

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Dini ya zamani inayofahamika kama Marapu, ni maarufu sana eneo la Sumba mbali na Ukiristo na Uislamu. Ili kuweka dunia sawa, kulingana na dini hiyo, miungu hufurahishwa kwa sherehe fulani na kutoa sadaka.
“Eneo la Sumba, watu wanaaamini kwamba maji yanapogusa paji lako la uso huwezi kuondoka tena kwenye nyumba hiyo,” Citra amesema. “Nilifahamu fika kinachoendelea, waliponifanyia utamaduni huo niligeuka dakika za mwisho ili maji yasiniguse kwenye paji langu la uso.”
Waliomteka walimuambia mara kadhaa kwamba wanachofanya ni kwasababu ya mapenzi na kuwa ni kwa ajili yake ili aweze kuolewa.
“Nililia hadi koo yangu ikakauka. Nikagaragara chini. Niligonga gonga funguo ya pikipiki niliyokuwa nimeshika kwa tumbo langu hadi ikaharibika. Niligonga kichwa changu dhidi ya nguzo kubwa za mbao. Nilitaka waelewe kwamba siko radhi na wanachokifanya. Nilitumai pengine wangenionea huruma.”,
Kwa sita zilizofuata, alikuwa amewekwa ndani yaani ni kama gereza ndani ya nyumba na kulala sebuleni.
“Nililia usiku mzima, na sikulala. Nilihisi kama ninakufa.”
Citra alikataa kula na hakunywa chochote alichopewa na familia hiyo akiamini kwamba hilo lingewafanya kupata laana: “Ikiwa tutakula chakula chao, ni sawa na kwamba tumekubali kuolewa.”
Dada yake alikuwa akimpelekea chakula kisiri na maji huku familia yake kwa usaidizi na makundi ya haki za wanawake wakiwa wanajadiliana kuachiliwa kwake na viongozi wa kijijini na familia ya anayetarajiwa kuwa mume wake.

Hakuna fursa ya kujadiliana
Kundi la haki za wanawake la Peruati yamehifadhi kesi saba za mabibi harusi waliotekwa nyara kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, na kuna inami kuwa kuna harusi nyingi ambazo zimefanyika katika maeneo ya vijijini ya kisiwa hicho.
Wanawake watatu tu, akiwemo Citra, hatimae waliachiliwa huru. Katika visa vya hivi karibuni vilivyonaswa kupitia video mwezi Juni, mwanamke mmoja alisalia kwenye ndoa.
“Walisalia kwasababu hawakuwa na cha kufanya,” amesema mwanaharakati Aprissa Taranau, kiongozi wa eneo Peruati. “Kawin tangkap wakati mwingine inaweza kupangwa na wanawake huwa hawana tena fursa ya kujadiliana.”
Anasema kuwa wale wanaofanikiwa kuondoka katika ndoa hizo zilizopangwa mara nyingi huwa wanatengwa na jamii zao.

“Huwa wanachukuliwa kama aibu na watu wanasema hawataweza tena kuolewa kwa kipindi hicho au kuwa na watoto. Hivyobasi wanawake wengi wanasalia kwenye ndoa za namna hiyo kwa kukosa la kufanya.,” Citra anasema.
Yeye mwenyewe hicho ndicho alichoambiwa.
“Namshukuru Mungu sasa hivi nimeolewa na mchumba wangu na tuna mtoto wa mwaka mmoja,” amesema kwa kutabasamu, miaka mitatu sasa tangu alipotokewa na tukio hilo la kuhuzunisha.
Ahadi ya kumaliza utamaduni huo
Wanahistoria na mkuu wa kijiji Frans Wora Hebi alidai kwamba utamaduni huo ni sehemu utajiri wa Sumba na kuongeza kwamba unatumiwa na watu kulazimisha wanawake kuolewa bila idhini yao.
Ukosefu wa hatua stahiki na viongozi wa maeneo na serikali kuna maanisha kwamba utamaduni huo utaendelea, anasema.
“Hakuna sheria inayopinga utamaduni huo, mbali na kwamba wakati mwingine wale wanaoutekeleza hukemewa na jamii lakini hakuna sheria au utamaduni unaopinga tabia hii.”
Baada ya malalamiko ya umma, viongozi wa kidini huko Sumba walitia saini azimio linalopinga utamaduni huo mapema mwezi huu.

Waziri wa kuwezesha kina mama Bintang Puspayoga alitembelea kijiji hicho kutoka mji wa Jakarta na kuhudhuria mkutano.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mkutano: “Tumezungumza na viongozi wa eneo na wa kidini, utamaduni wa kuteka wanawake na kuwaoza uliosambaa mitandaoni kwa njia ya video sio utamaduni wa Sumba.”
Aliahidi kwamba azimio hilo ndio mwanzo wa juhudi za serikali za kumaliza utamaduni huu aliouelezea kama dhulma dhidi ya wanawake.
Makundi ya kutetea haki za wanawake yalifurahishwa na hatua hiyo lakini wakaielezea kama hatua moja ya safari ndefu.
Citra anasema anashukuru kwamba sasa serikali imeanza kuchukulia suala hilo kwa uzito mkubwa na kutumai kuwa matokeo yake hakuna ambaye atapitia tena alichopitia yeye.
“Kwa wengine huenda huu ukawa ni utamaduni wa mababu zetu. Lakini umepitwa na wakati kwasababu unadhuru vibaya wanawake.”
The post Hii ndio nchi ambayo wanawake hutekwa nyara ili wakaolewe appeared first on Bongo5.com.