Na Ahmad Mmow, Lindi.

Wakati joto la uchaguzi likizidi kupanda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika jimbo la Lindi kimeanza kuonesha kwa dhati kwamba kinalitaka jimbo hilo kwanafasi ya ubunge. Baada ya kada wake, Hemed Ali kuchukua nakurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea.

Akizungumza baada ya kuchukua, kujaza, kupata wadhamini na kurejesha fomu, Hemed alisema  yeye alitafakari na kupima mambo mengi yaliyo ndani na nje ya chama akabaini kwamba anasababu ya kuomba ridhaa ya chama chake kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo la Lindi.

Hemed alisema wanachama wanaotakiwa kiteuliwa kugombea nafasi za uongozi wa umma kupitia chama hicho niwale ambao wameiva kiitikadi na kifalsafa ili wawe wawakilishi wazuri wa wananchi na chama hicho. Sifa ambazo yeye anaamini anazo.

Aidha Hemed aliweka wazi kwamba yupo tayari kumuunga mkono mwanachama yeyote atakayeteuliwa na chama hicho kuwa mgombea wake wa ubunge wa jimbo hilo. Kwani mchakato wa kura za maoni wanatakiwa kuwa na nia moja tu, ambayo ni kukifanya chama hicho kishinde.

Kwaupande wake katibu wa jimbo la Lindi, Zingatia Seleman ambae alitoa na kupokea fomu hiyo toka kwa Hemed aliwaasa watia nia wote wazingatie taratibu na sheria. Pia waepuke vitendo vya rushwa.

Kuhusu waliochukua na kurejesha fomu za ubunge hadi mchana alikuwa ni Hemed Ali pekee. Hatahivyo, Zingatia alisema anaamini hadi saa kumi alasiri ya leo kuna uwezekano wa idadi hiyo kuongezeka. Kwani fomu zimechukuliwa kwa njia ya mtandao.

Kuhusu nafasi ya udiwani, Zingatia alisema hadi sasa waliochukua fomu za udiwani wa kata ni 11 na viti maalumu ni 8.

Mlango wa kuchukua fomu za ubunge ulifunguliwa tarehe 4/7/2020 na utafungwa leo saa 10.00 alasiri. Wakati mlango wa kuchukua fomu za udiwani utafungwa tarehe 17/7/2020. Ambapo zoezi la kuchukua na kurejesha fomu linafanyika katika ofisi ya jimbo la Lindi iliyopp katika manispaa ya Lindi.