Meli iliyowaokoa wahamiaji katika bahari ya Mediterania imetangaza hali ya hatari jana baada ya abiria wake sita kujaribu kujiuwa na mapigano yalizuka ndani ya meli hiyo. 

 Hali ndani ya meli hiyo ya Ocean Viking inaendelea kuwa mbaya baada ya kukataliwa ama maombi ya kutia nanga kupuuzwa kutoka bandari saba nchini Italia, na Malta licha ya kubeba wahamiaji 180, kituo cha kupokea taarifa za maafa katika bahari ya Mediterania kimesema katika taarifa. 

 Baada ya maombi saba kwa ajili ya sehemu ya usalama kwa mamlaka husika za usafiri wa majini katika muda wa wiki moja iliyopita na majaribio sita ya kujiuwa yaliyofanywa katika masaa 24, Ocean Viking imetangaza hali ya hatari, kundi hilo limeandika. 

 Mapema jana, mtu mmoja alijaribu kujinyonga, wakati wengine wanaonesha ishara za matatizo makubwa ya kiakili, sononeko na hali mbaya ambayo imezusha mapigano kadhaa miongoni mwa walionusurika ndani ya meli hiyo, SOS Medieterania imesema.