Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hasaan Abbasi ametoa saa 24 kwa Bodi na Menejimenti ya Chama cha Hakimiliki na Haki Shirikikishi Tanzania (COSOTA) kuwasilisha mkakati wa namna Wasanii watakavyonufaika kupitia Taasisi hiyo.

Katibu Mkuu ametoa agizo hilo jana  Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya makabidhiano ya chama hicho kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara anayoisimamia.

“Tumshukuru Rais John Magufuli kwa sababu mjadala wa kwa nini COSOTA ipo Wizara ya Viwanda na Biashara umekuwa mrefu, lakini ndani ya saa 24 tangu Julai 12, 2020 Rais aliweza kusaini Waraka wa kuihamishia Wizarani kwetu”, Dkt. Abbasi.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo inatakiwa kuhakikisha kuwa inawasaidia wasanii katika kusimamia haki zao ili kuondokana na umaskini na kufikia malengo waliyojiwekea katika kazi zao za Sanaa kwani ni jukumu la taasisi hiyo kuhakikisha kuwa inamsaidia msanii kutoka kuwa msanii maarufu maskini na kuwa msanii maarufu tajiri.

Aidha, Dkt. Abbasi aliongeza kuwa taasisi hiyo kuhamia Wizara ya Habari ni jambo jema katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Idara ya Maendeleo ya Sanaa kwa kuhakikisha wasanii wanapata huduma kwa wakati na chini ya mwamvuli mmoja.

Dkt. Abbasi alieleza kuwa kwa sasa kuna mabadiliko na mafaniko mengi katika sekta ya Sanaa ambapo Juni 26, 2020 Wizara ilifanikiwa kutangaza Kanuni za Filamu na Michezo ya Kuigiza kupitia gazeti la Serikali namba 488 ambapo kuna manufaa mengi kwa wasanii ikiwemo kupungua kwa tozo za filamu kutoka shilingi 500,000/= hadi shilingi 50,000/= lengo ikiwa ni kuwawezesha kutengeneza filamu zenye ubora.

Vile vile faida nyingine ya kanuni hizo ni kuwepo kwa kamati ya kutetea haki za wasanii ambapo Serikali imefanikiwa kurejesha kiasi cha milioni 200 ambapo kati ya hizo, shilingi milioni 65 zilirejeshwa kwa familia ya marehemu Mzee Majuto pamoja na kiasi cha milioni 20 zilirejeshwa kwa familia ya marehemu Steven kanumba kutoka katika kampuni ambazo ziliingia mikataba na Wasanii hao.

Naye Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe ameutaka uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Habari katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji wa COSOTA, Doreen Sinare ameahidi kusimamia kwa ufanisi majukumu ya taaasisi hiyo inayosimamia haki miliki pamoja na kusajili wabunifu kukusanya na kugawa mirabaha na kusuluhisha mogogoro inayohusiana  na haki miliki pamoja na kutoa ushauri.

Nao baadhi ya wasanii walitoa maoni yao kuhusiana na makabidhiano haya ambapo Msanii wa Filamu na Michezo ya kuigiza, Vyonne Cherrie (Monalisa) ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa kuhamishwa kwa taasisi ya COSOTA kwenda Wizara ya Habari kwani imeepusha milolongo mingi ya ufuatiliaji wa kazi za filamu na sanaa.

Huku Msanii wa Muziki wa kizazi kipya, Kala Jeremiah alisema kuwa ulinzi na ulezi wa sanaa unatakiwa kwenda pamoja hivyo ni jambo jema kwa COSOTA kuhamia Wizara ya Habari ili waweze kufanya kazi kwa ushrikiano na BASATA.