Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema raia milioni 25 nchini humo tayari wamepata maambukizi ya virusi vya corona na wengine milioni 35 wako katika hatari ya kuambukizwa.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya nchini humo, ametahadharisha kuwa nchi hiyo itahitaji idadi mara mbili zaidi ya vitanda. Mpaka sasa, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa ni 269,440.

Rouhani alisema: ”Ikiwa tutaitegemea ripoti hii,ambayo inasema watu milioni 25 nchini mwetu wameathirika na pengine idadi yote iliyobaki , karibu milioni 35 zaidi watapata maambukizi miezi ijayo, ripoti hiyo hiyo inakisia kuwa idadi ya watkaolazwa miezi ijayo inatarajiwa kuwa mara mbili zaidi ya ile tuliyoishuhudia siku 150 zilizopita.”

Rouhani amesema watu 14,000 wamepoteza maisha kutokana na janga la virusi vya corona na 200,000 walilazwa hospitalini katika kipindi cha siku 150 zilizopita, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Misikiti kote nchini Iran ilifunguliwa miezi miwili iliyopita licha ya kwamba baadhi ya maeneo bado yalikuwa yameathirika vibaya na janga la virusi vya corona.

Mikusanyiko ya kufanya sala ilikuwa imerejea katika miji 180 yenye kuonekana kuwa na kiwango cha chini cha hatari ya kupata maambukizi baada ya kukatizwa kwa miezi miwili kulingana na kituo cha habari cha taifa hilo.

Iran pia iliondoa marufuku ya kusafiri baina ya miji na majengo ya kibiashara huku shughuli za kibiashara zikiwa zimerejelelewa.

Iran, moja ya maeneo ya Mashariki ya Kati yaliyoathirika vibaya na virusi vipya vya corona ilianza kulegeza masharti na kurejelelea maisha ya kawaida ili kufufua uchumi ambao tayari unakumbana na vikwazo vya Marekani.

Hata hivyo maafisa wa afya walionya kwamba kulegeza masharti kunaweza kusababisha wimbi jingine la maambukizi ya virusi vya corona.

The post Corona yaliangamiza taifa la Iran, watu milioni 25 wapata maambukizi appeared first on Bongo5.com.