Marekani imeiamuru China ifunge ubalozi wake mdogo uliopo mjini Houston, Texas, kufikia Ijumaa-hatua iliyoelezewa kama “uchokozi wa kisiasa ” na Beijing.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa uamuzi huo unalenga “kulinda akilimiliki ya Wamarekani “.

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uchina Wang Wenbin amesema kuwa uamuzi huo “ni wa kushitua na usio na sababu “.

Taarifa hii imekuja baada ya watu wasiojulikana kuchukuliwa video wakichoma karatasi katika pipa la taka katika eneo la jingo.

Hali ya wasiwasi imekua ikiendelea kuongezeka baina ya Marekani na China kwa muda.

 

Utawala wa rais Donald Trump umekuwa na sintofahamu ya mara kwa mara na ule wa Beijing juu ya biashara na janga la virusi vya corona, pamoja na hatua ya Uchina kuweka sheria mpya ya usalama juu ya Hong Kong.

Halafu Jumanne, wizara ya sheria ya Marekani iliishutumu China kwa kudhamini wadukuzi ambao wamekuwa wakilenga maabara zinazotengeneza chanjo za Covid-19.

Ni kwanini Marekani inasema inaufunga ubalozi mdogo wa China?

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa taarifa muda mfupi baada ya Bwana Wang kuzungumza Jumatano.

” Tumeagiza kufungwa kwa ubalozi mdogo wa PRC [Jamuhuri ya watu wa China] Houston, ili kulinda Akilimiliki ya Wamarekani na taarifa za kibinafsi za Wamarekani ,” Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bi Morgan Ortagus alisema.

Ubalozi mdogo wa China wa Houston ni moja ya balozi ndogo tano za China zilizopo nchini Marekani, bila kuhesabu Ubalozi wake uliopo Washington DC. Haijawa wazi kuhusu iwapo ubalozi huu pia umetajwa miongoni mwa zile zilizoamrishwa kufungwa.

Bi Ortagus aliongeza kuwa Marekani “haitavumilia ukiukaji wa hadhi ya nchi yetu na vitisho vya Jamuhuri ya Watu wa China (PRC) na kama tu ambavyo hatukuvumilia, utendaji wa biashara usio wa haki wa haki , wizi wa kazi za Wamarekani, na tabia nyingine za uchokozi “.

Bi Ortagus pia alitaja makubaliano ya Vienna kuhusu mahusiano ya kidiplomasia , ambayo yanasema nchi “zina wajibu wa kutoingiliana kuhusu masuala ya ndani” ya nchi mwenyeji.

Katika taarifa tofauti, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliishutumu China kwa kuhusika “katika ujasusi mkubwa kinyume cha sheria na kushawishi utendaji “, kuingilia “siasa za ndani ” pamoja na “kuwatisha wafanyabiashara wakuu, kuzitisha familia za Wamarekani wanaoishi China, na tuhuma nyingine zaidi “.

Je China ilipokea vipi agizo hilo?

China ilitaja uamuzi huo kama uchokozi wa kisiasa , ikisema kuwa unakiuka sheria ya kimataifa .

Bwana Wang aliendelea kusema kwamba Washington imekuwa ikiilaumu China kupitia ‘unyanyapaa’ na ‘kuishambulia’ mara kwa mara.

Aliitaka Marekani kufikiria , akisema kuwa iwapo itasisitiza kufuata mkondo huo wa mbaya , ”China italipiza kwa kuchukua hatua kali zaidi.”.

Liu Xiaoming asema China sio adui wa Marekani
,Liu Xiaoming asema China sio adui wa Marekani

“Ukweli ni kwamba , kutokana na idadi ya balozi za China na Marekani pamoja na idadi ya balozi ndogo katika mataifa hayo mawili pamoja na idadi ya wafanyakazi katika balozi hizo , Marekani ina wafanyakazi wengi zaidi wanaofanya kazi nchini China”, bwana Wang alisema.

Chombo cha habari nchini China Global Times kilianza kufanya kura ya maoni ambapo balozi ndogo za Marekani zilitarajiwa kufunga mara moja.

Baadaye wizara ya masuala ya kigeni ilichapisha onyo kwa wanafunzi wa China nchini Marekani , ikiwataka kuwa macho kwa kuwa vitengo vya usalama nchini Marekani vimeanza kuwahoji , kuwanyanyasa na kuwapokonya mali zao wanafunzi wa China wanaosomea nchini Marekani.

The post China yapewa siku mbili kufunga ubalozi wake mdogo Marekani, Sababu zaelezwa appeared first on Bongo5.com.