Dar es Salaam. Watanzania sasa wanaweza kufanya malipo ya kodi na yasiyo ya kodi kwenda kwa taasisi zaidi ya 600 za serikali wakiwa ndani ya matawi yote ya Benki ya UBA kwa haraka zaidi, imeelezwa.
Hili imetokana na uamuzi wa Serikali kuiunganisha Benki ya UBA na mfumo wa malipo wa Serikali wa kielektroniki (GePG).

UBA ilitangaza jijini Dar es Salaam jana kuwa imepata kibali cha kuwa moja kati ya benki nane nchini zinazotumika katika kufanya malipo ya kodi na yasiyo ya kodi kwenda kwa taasisi za serikali kupitia mfumo wa GePG.

Mkuu wa kitengo cha sekta ya umma wa Benki ya UBA, Bw. Dominick Timothy alisema kuwa kuunganishwa kwa benki yake katika mfumo wa GePG ni moja wapo ya njia za taasisi hiyo ya fedha kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania, chini ya Rais John Magufuli.

Alisema kutokana na kuunganishwa kwa UBA na mfumo wa GePG, Benki hiyo sasa itaoanisha mfumo huo na njia zake za kidijitali zakibenki.
Njia hizo ni pamoja na kupata huduma za benki kwa njia ya simu (Mobile App), huduma za benki kwa njia ya mtandao (internet banking) pamoja na njia zijulikanazo kama Leo chatbot, USSD Magic Banking na Webcollect.

Lengo la kuunganisha na njia hizo zakibenki ni ili kuwawezesha Watanzania kuweza kufanya malipo ya serikali popote pale walipo pasipo kulazimishwa kwenda katika tawi la benki.

“Siku zote, hamu yetu imekuwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo Watanzania. Kwa njia hii, tunaunga mkono juhudi za serikali katika kukusanya mapato kwa njia za kidijitali. Tunaishukuru Serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wizara nzima ya Fedha na Mipango kwa kutupatia nafasi hii ya kuwatumikia Watanzania,” alisema.

Alisema mtu yeyote anaweza kufanya malipo ya serikali kwa njia ya GePG bila kujali kama ni mteja wa Benki ya UBA au laa.

Mfumo wa GePG unasaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za Umma.
Faida za mfumo huo kwa taasisi za umma ni pamoja na urahisi katika usuluhishi wa miamala na usuluhishi wa taarifa za kibenki pamoja na kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo.

Mfumo pia unapunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji wa Fedha za Umma.

Serikali ilianza kutumia mfumo wa GePG mwaka 2017 ikiwa ni njia moja wapo ya Serikali, chini ya Rais Magufuli, kudhibiti upotevu wa pesa za umma.
Benki ya UBA imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuiendeleza Tanzania ambapo mwaka jana benki hiyo ilijiunga na benki nyingine kutoa dhamana za benki ili kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji.

Mradi huo wenye thamani ya $2.95 billion utafua umeme wa Megawati 2,115.