Serikali imesema katika kuhakisha tatizo la sumukuvu kwenye mazao ya wakulima linapatiwa ufumbuzi elimu kwa wakulima ni muhimu kutolewa.
 
Kauli hiyo imetolewa leo wilayani Kiteto na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alipofungua mafunzo ya udhibiti sumukuvu kwa wakulima wa kijiji cha Engusero kwa niaba ya vijiji  vingine 28.
 
Bashe amesema wakulima wanapaswa kuelimishwa zaidi kutambua namna ambavyo mazao yao hususan mahindi na karanga yanavyoweza kuchafuliwa na sumukuvu ili waweze kudhibiti kwani tatizo hili linasababisha hasara kwa mazao yao na pia afya za binadamu.
 
Bashe alipongeza mradi wa kudhibiti sumukuvu (TANIPAC) kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wakulima ili watambue namna sahihi ya kukabiliana na tatizo la sumukuvu.
 
“ Mkulima ndio mgani namba moja,hivyo ukimfundisha kanuni bora za kilimo ataweza pia kuwafundisha wakulima wenzake” alisisitiza Bashe
 
Naibu Waziri Bashe aliongeza kusema kuwa wakulima kupitia mradi wa TANIPAC watajifunza kutambua namna mazao yao yanavyoweza kuchafuliwa na fangasi wanaosababisha sumukuvu katika vijiji vyao ikiwemo kutoweka mahindi chini ya ardhi.
 
Akiwa katika ukaguzi wa shamba la mfano la mahindi kijiji cha Engusero Naibu Waziri huyo alijionea jinsi mahindi yalivyoanza kuharibiwa na wadudu kufuatia kuchelewa kuvunwa  na kuagiza kuwa wataalam wa wizara waandae kalenda ya Kilimo
 
“TANIPAC andaeni kalenda ya Kilimo ikionesha mkulima aanze lini kupanda,kupalilia,kuweka mbolea na muda gani ni muaka kuvuna mahindi .Hii ikifanyika itapunguza mathara kwa wakulima wa Kiteto na maeneo mengine kulingana na ikolojia” alisema Bashe
 
Alisema serikali pia itajenga kituo cha umahiri eneo la Kibaigwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima wengi zaidi kupata taaluma ya shughuli za Kilimo “VETA ya Kilimo”
 
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa kudhibiti Sumukuvu Clepin Josephat alisema mafunzo hayo yanafanyika  katika wilaya nne za Kiteto, Babati, Kondoa na Chemba ambapo wanalenga kuwafikia wakulima 1400 katika siku nane za mafunzo hayo
 
Clepin aliongeza kuwa mradi huo utajenga ghala la kisasa la kuhifadhia mazao ya nafaka litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 2000 katika kijiji cha Engusero wilaya ya Kiteto lenye ukubwa wa ekari 10,000.
 
“ Tunapaswa kuamini kuwa madhara ya sumukuvu yapo,tujitokeze kupata elimu.Fangasi wa kuvu wanaishi ardhini wakulima epukeni kuweka mahindi na karanga chini baada ya kuvuna ili wadudu wasiweze kuathiri mazao yenu ” alisema Clepin 
 
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Bashe alikagua shamba la mkulima  wa mahindi na kisha aliongea na wananchi wa kijiji cha Engusero ambapo walielezea kero ya bei ya mbegu za mahindi na alizeti kuwa zipo juu hivyo wakulima kushindwa kuzinunua.
 
Katika hatua nyingine Bashe aliagiza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini ambapo miradi ya TANIPAC inafanyika watoe ardhi bure bila kudai fidia kama ilivyofanyika kwa wilaya ya Kiteto
 
“ Hakuna kulipa fidia kwa miradi ya TANIPAC ,hivyo halmashauri itakayodai fidia ya ardhi ondoeni mradi na kupeleka wilaya nyingine” alisisitiza Naibu Waziri Bashe.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Tamimu Kambona aliwasihi wakulima wanaoshiriki mafuzo kutokwepa gharama katika kuhifadhi mazao yao ili yasichafuliwe na sumukuvu hali itakayoathiri upatikanaji bei nzuri sokoni.
 
“ Tatizo kwenye wilaya yetu ya Kiteto lipo kubwa na linasababisha hasara sana kwa wakulima hivyo lazima tuwafundishe wakulima kanuni bora za Kilimo na kuepuka sumukuvu “ alisema Kambona
 
Wilaya ya Kiteto katika msimu huu inatarajia kuvuna mahindi tani 270,000 tofauti na tani 160,000 za msimu wa 2019/20 kutokana na uwepo wa hali ya hewa nzuri na usimamizi wa wataalam wa Kilimo. 

Mwisho
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
KITETO
07.07.2020