Klabu ya Aston Villa imemfuta kazi mkurugenzi wake wa michezo , Jesus Garcia Pitarch baada ya kukosoa sera za usajili za klabu hiyo.

Pitarch aliondoka klabuni hapo siku ya jumatatu ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kufanikiwa kusalia katika ligi kuu ya England baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United.

Ilifahamika kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Dean Smith alihakikishishiwa kibarua chake na kuahidiwa kiasi cha fedha kwa ajili ya usajili ingawa klabu ilishaanza kufanya tathmini ya msimu uliomalizika na mikakati ya msimu ujao.

Smith ndiye aliyependekeza usajili wa Tyrong Mings na Tom Heaton ambao walikua na matokeo chanya katika klabu hiyo.

Katika majira ya kiangazi, Villa ilitumia kiasi cha pauni milioni 140 katika usajili huku Pitarch akiwa ndiye aliyehusika katika kuleta wachezaji wakiwemo Wesley Moraes aliyenunuliwa kwa ada ya rekodi ambayo ni pauni milioni 21,Matt Targett,Douglas Luiz ,Marvelous Nakamba na Mbwana Samatta.

Pitarch pia alihusika katika usajili wa Trezeguet raia wa Misri ambaye alifunga mabao matatu katika mechi chache za mwisho zilizoinusuru Villa kuporomoka daraja.

Si taarifa nzuri kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye tangu asajiliwe kwa ada ya pauni milioni 8 kutoka KRC Genk katika dirisha la usajili la mwezi Januari mwaka huu, amecheza mechi 16 za mashindano yote na kufunga mabao 2 tu.

The post Aliyefanikisha usajili wa Samatta atimuliwa Aston Villa appeared first on Bongo5.com.