Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia njia za tiba asili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona na kudhibiti magonjwa mengineyo ya kuambukiza.
Prof. Makubi ametoa wito huo jana alipofanya ziara ya kuona hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma.
“Katika kudhibiti ugonjwa wa corona wananchi walipokea kwa mikono miwili mbinu za kuepuka kuambukizwa ugonjwa wa corona ikiwemo unawaji mikono kwa maji yanayotirika na sabuni, uvaaji wa barakoa, kuepuka mikusanyiko na misongamano pamoja na mbinu za tiba asilia/tiba mbadala ili kutibu ugonjwa wa corona”. Amesema Prof. Makubi
Pamoja na kupungua kwa ugonjwa wa corona nchini, Prof. Makubi amesema kuwa bado Watanzania tunatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kinga ili hatimae tuweze kutokomeza kabisa ugonjwa wa corona au pale ambapo bado utaendelea kuwepo tuweze kuishi nao bila madhara makubwa.
Prof Makubi amesema kuwa Serikali inawapongeza wananchi kwa kuipokea na kutumia njia ya tiba asili/mbadala katika kusaidia kutibu ugonjwa wa corona njia ambayo imeonekana kuimarisha kinga dhidi ya Ugonjwa huo pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza na kuwataka wananchi kuendelea na mbinu walizoelimishwa kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.
“Mwamko tulio nao sasa hivi wananchi juu ya mbinu hizi tusiziache, tukiendelea nazo zitatusaidia kujikinga na magonjwa mengine” amesisitiza Prof. Makubi.
Hatukuwa na utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara, lakini tuelewe pia usafi wa mikono unatusaidia pia kupunguza hatari ya kupata magonjwa mengine yanayotokana na uchafu yakiwemo magonjwa ya kuhara, au hata kipindupindu.
Hata hivyo Prof. Makubi hakusita kumshuruku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuelekeza bajeti ya tiba asili/mbadala na tafiti za dawa asilia iweze kuongezwa ili kuwawezesha wataalam wanaotengeneza dawa hizo zinazosaidia kutibu magonjwa mbalimbali na kupambana na maambukizi ya virusi vya corona nchini.
Aidha Prof Makubi amewaagiza wataalam wa afya hasa Wakurugenzi, Waganga wa Mikoa, Wilaya, Maafisa wa afya ngazi za jamii, viongozi wa mashule, vyuo, michezo, na mamlaka za mitaa kuendelea kutoa elimu ya kupambana ugonjwa wa corona na kuendelea kuhamasisha mbinu za kuthibiti CORONA ambazo zikiendelezwa zitapunguza uwezekano wa kuibuka magonjwa mengine hivyo kuokoa afya za wanachi na fedha nyingi ambazo zingetumika kutibu wagonjwa.