Kufuatia Rais Dk John Magufuli jana kutangaza kufungua Shule zote ifikapo Juni 29, leo Waziri wa @wizara_elimutanzania, Prof Joyce Ndalichako ametangaza ratiba ya masomo na mitihani kwa ajili ya kukamilisha mwaka wa masomo.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ndalichako amesema muhula wa kwanza wa masomo utamalizika Agosti 28 mwaka huu na kuanza kwa muhula mpya utakaoishia Desemba 18 mwaka huu.

Prof Ndalichako amesema ili kukamilisha muhtasari wa masomo shule zitalazimika kuongeza saa mbili za masomo kwa siku ili kufidia muda uliopotea ambapo maelekezo ya kuongeza muda huo hayatahusisha madarasa ya awali.

“Tangu tumefungua Shule na Vyuo Juni 1, tumekuwa tukifuatilia afya za wanafunzi wetu na mpaka Juni 16, hatujapokea kisa hata kimoja cha Mwanafunzi aliyepata Virusi vya Corona, hivyo muhimu sana kuendelea kuchukua tahadhari” amesema Waziri wa mu, Prof Ndalichako.

Aidha Waziri Ndalichako ametoa ratiba ya mitihani kama ifuatavyo,”Darasa la 7 wataanza mitihani yao Oktoba 7-8, Kidato cha 2 wataanza mitihani yao Novemba 9 hadi Nov 20, wanaomaliza Kidato cha Nne na wa kujitegemea na wale wanaofanya mitihani ya maarifa, wataanza Novemba 23 hadi  Disemba 11, na Darasa la Nne wataanza Novemba 25 – 26, 2020″.

Chanzo Michuzi

The post Waziri wa Elimu Prof Ndalichako, atangaza ratiba za mitihani na masomo rasmi appeared first on Bongo5.com.