Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaambia Askari wa Usalama Barabarani kwamba, wakiona Daladala imesimamisha abiria ambao si wanafunzi kwa kipindi hiki waikamate kwa kuwa agizo la 'level seat' bado halijatenguliwa.


Makonda ameyabainisha hayo leo Juni 2, 2020 wakati akitoa ruhusa kwa madereva na makondakta wa daladala, kuhakikisha wanasimamisha wanafunzi ambao hawatozidi wanne, kwa kuwa wao hawana uwezo wa kulipia nauli yote na kwa kufanya hivyo watawawezesha kuwahi mashuleni kwao.

"Suala la level seat lipo pale pale wazingatie, lakini wanapokuja kwenye point ya wanafunzi hawana sababu ya kumuacha kwa sababu hana pesa ya kulipa kama mtu mzima, wanafunzi wanne wakisimama ndani ya daladala si dhambi, kwahiyo Traffic mlioko barabarani mkikuta gari limebeba wanafunzi wamesimama wanne msilikamate ila mkikuta limesimamisha abiria kamateni hiyo ni halali yake" amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa suala la kusimamisha wanafunzi wanne ndani ya daladala linaanza rasmi leo.