SALVATORY NTANDU
Wananchi zaidi ya 2000 wanaoishi Pembezoni mwa mji wa Kahama mkoani Shinyanga wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya kukamilika kwa miradi mitatu ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) iliyogharimu ya shilingi milioni 686  fedha za Mapato ya ndani.

Kauli hiyo imetolewa June 3,2020 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka hiyo Mhandisi  Allen Marwa wakati akitoa ufafanuzi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kahama iliyotembelea na kukagua ujenzi wa miradi hiyo inayotekelezwa na KUWASA.

Miradi hiyo ni pamoja na Mwamva  hadi Mbulu, Chapulwa na Mhungula Mlimani ambayo imekamilika kwa asilimia 99 imetumia fedha kidogo ikilinganishwa na hapo awali ambapo zilikuwa imetengewa shilingi Milioni 981hadi kukamilika kwake.

“Tutahakikisha huduma za maji zinawafikia wakazi wote wa wilaya ya kahama na hivi sasa tunaongeza mtandao wa maji katika kata zilizopopembezoni mwa mji sambamba na kutoa elimu kuhusiana na matumizi ya maji safi sana salama kwao,”alisema Marwa.

Marwa alifafanua kuwa miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 99 nawameweza kuokoa fedha zaidi ya shilingi milioni 290 fedha za mapato ya ndani endapo mradi huo ungetekelezwa na Mkandarasi ambaye hapo awali Wizara ya Maji ilizuia kupewa kandarasi hiyo na kuagiza watekeleze KUWASA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo Anamringi Macha alisema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuondoa kero kwa wananchi kutafuta huduma hiyo umbali mrefu na kushindwa kufanya kazi za kuzalisha mali katika maeneo yao.

“KUWASA mmeitekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwa kuhakikisha kata 15 zilizopo katika halmashauri ya Mji wa kahama zinapata huduma hii muhimu,hongereni na eneleeni kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na uzalendo,”alisema MACHA.

Debora Morisi ni Mkazi wa Mhungula Wilayani humo ameishukuru serikali kuwapatia huduma hiyo na kusema kuwa hapo awali walikuwa wanafuata maji umbali mrefu visimani  amabayo sio safi wala salama ambayo yalikuwa yanauzwa kwa bei ya shilingi mia 200 hadi 500 kwa kipindi cha kingazi.

“Kwa sasa tunanunua maji kwenye Magati kwa shilingi 50,hakika serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli ni sikivu imeweza kusikiliza kilio chetu cha Muda mrefu cha maji ambapo tulikuwa tunalazimika kwenda kutafuta maji usiku na tunakutana na wanayama wakali aina ya fisi,”alisema Morisi.