Wabunge 21 na madiwani 09  wa CUF,waliomaliza muda wao, wakiongozwa na Ally Salehe, Mbunge wa Malindi Visiwani Zanzibar, kumejiunga na ACT-Wazalendo.

Wabunge hao wastaafu wamepokelewa leo Jumamosi tarehe 20 Juni 2020 jijini Dar es Salaam, na viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, akiwemo Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wake na Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama hicho.

Wimbi la wanachama wa CUF kutimkia ACT-Wazalendo ,limeshika kasi tangu mwezi Machi mwaka 2019, baada ya kuibuka kwa mgogoro wa kiuongozi baina ya Maalim Seif , aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, na Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge hao, Salehe amesema wamejiunga na chama hicho baada ya kuona CUF imepoteza nguvu ya kuhimiri vishindo vya siasa

Salehe amesema wanaanza upya ndani ya ACT-Wazalendo, huku akijigamba kwamba wamejipanga kutetea majimbo yao kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Aidha, Salehe amesema walitamani kujiunga na ACT-Wazalendo pamoja na Maalim Seif na wafuasi wake kupitia kampeni ya ‘Shusha Tanga, Pandisha Tanga’, lakini walishindwa kutokana na sababu zilizookuwa nje ya uwezo wao.