Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Viongozi wa dini  jijini Dodoma wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake uliotukuka.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Askofu wa Kanisa la EAGT  Ipagala jijini humo, Evance Chande alisema kuwa Rais John Pombe Magufuli ni kiongozi mwenye uthubuti, mwenye kufanya maamuzi magumu ambayo yamesaidia katika utekelezaji na usimamizi  wa miradi mbalimbali kama vile  ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, ununuzi wa ndege mpya 11, ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa pamoja na soko katika jiji la Dodoma, ikiwa ni baadhi ya miradi  aliyotekeleza.

“Kutokana na mafanikio haya yametufanya tushindwe kukaa kimya  hivyo tumelazimika kuja kutoa tamko la kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi hiki cha miaka mitano, ambapo kila mmoja wetu hapa amefuatilia kwa makini hotuba yake ya Juni 16 mwaka huu,” alisema Askofu Chande

Askofu Chande anaongeza kuwa tangu mgonjwa wa kwanza aliyeathirika na virusi vya homa kali ya mapafu (Covid-19) alipogundulika nchini mwezi Machi mwaka huu,Rais Magufuli alionesha ujasiri, weledi na uthubutu katika kupambana na ugonjwa wa  Covid-19. huku ukiwa ni ugonjwa mpya na hapakuwa na uzoefu wowote kutoka katika nchi nyingine duniani.

Aliongeza kuwa, katika kuonesha imani yake na haja ya Taifa katika  kumtegemea Mungu,  Rais Magufuli alilitangazia Taifa kufanya maombi ya siku tatu na kuwaomba viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika maombi hayo na hata baada ya maambukizi kupungua kwa kiasi kikubwa alitangaza tena maombi ya siku tatu kumshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga la Covid-19.

“Hadi tunatoa tamko hili Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa kwanza katika mataifa ya Afrika Mashariki kuruhusu Vyuo, Shule za Sekondari na Msingi kuendelea na masomo huku wakizingatia ushauri wa wataalamu wa afya” alisisitiza Askofu Chande.

Kwa upande wake, Katibu  wa mkoa na Mjumbe wa Baraza la Masheikh wa Mkoa wa Dodoma, Hussein Kuzungu alisema kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kufufua uchumi wa nchi sambamba na kukusanya kodi na kuitumia kutekeleza miradi mikubwa kwa lengo la kunufaisha watanzania.

Alitaja  baadhi ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kuwa ni kurejesha nidhamu ya uwajibikaji ndani na nje ya Serikali, uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi kwa lengo la kupambana na rushwa, madawa ya kulevya  sambamba na nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais unaotarajia kufanyika mwezi  Novemba mwaka huu, Sheikh Kuzungu alisema kuwa “tunatoa rai  kwa watanzania wote, kuzingatia kuwachagua viongozi wenye uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu na waadilifu ili Taifa letu liendelee kustawi.”