Rais Donald Trump amesema atapunguza nusu ya idadi ya wanajeshi wake walioko Ujerumani kwa sababu Ujerumani haitoi mchango wake kifedha ipasavyo ili kufadhili shughuli za Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Trump pia ameishutumu Ujerumani akidai haiishughulikii Marekani vyema kibiashara.
Rais Trump amewaambia waandishi wa habari mjini Washington Marekani, kwamba kuna wanajeshi 52,000 wa Marekani walioko Ujerumani na atapunguza idadi hiyo hadi 25,000.
Hata hivyo kulingana na makao makuu ya kijeshi ya Marekani Pentagon, idadi ya wanajeshi iliyotajwa na Trump inapotosha kwa sababu kuna kati ya wanajeshi 34,000 na 35,000 pekee wa kudumu walioko Ujerumani.
Wanajeshi wa Marekani wamekuwepo Ujerumani tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili duniani, ambapo walikuwa sehemu kubwa ya wanajeshi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO dhidi ya muungano wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi.
Kuibuka tena kwa malengo ya kijeshi ya Urusi chini ya Rais Vladimir Putin, kuliipa Marekani umuhimu wa wanajeshi wake kuwepo Ujerumani kwa miongo miwili iliyopita, huku nchi za kati na mashariki mwa Ulaya zikishinikiza kuimarishwa kwa ushirikiano thabiti na Marekani.
Trump amesema anataka kuadhibu kile alichokitaja kuwa mchango usiotosha wa Ujerumani kwa NATO, na kutumia suala la mustakabali wa wanajeshi, kama silaha ya kuunga mkono kitisho chake cha vita vya kibiashara na Umoja wa Ulaya.
Credit:DW
Credit:DW