TAMKO LA MHE. MUSSA AZZAN ZUNGU (MB.), WAZIRI WA NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA KWA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA KIMATAIFA YA SIKU YA KUPAMBANA NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA UKAME DUNIANI, TAREHE 17 JUNI, 2020

Ndugu Wananchi,
Kila mwaka tarehe 17 Juni, nchi yetu huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame. Kimataifa Maadhimisho ya Siku hii yanafanyika Jijini Seoul nchini Korea Kusini. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Tudhibiti Kuongezeka kwa Uzalishaji wa Chakula na Malighafi; Tukabiliane na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame” (Food. Feed. Fibre). Kaulimbiu hii inaelimisha jamii kuzalisha chakula na malighafi kwa njia endelevu ili kunusuru ardhi kutokana na hali ya Jangwa na Ukame. Aidha, Jamii inaelimishwa juu ya uhusiano wa Uzalishaji, Ulaji na Matumizi ya Ardhi.  

Ndugu Wananchi,
Maadhimisho ya siku hii yalitangazwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi Januari, mwaka 1995 kwenye Azimio namba 115. Azma ya maadhimisho haya ni Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani kama njia mojawapo ya utekelezaji wa shughuli za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (United Nations Convention to Combat Desertification) uliopitishwa mwaka 1992 ambapo nchi yetu ni mwananchama.

Ndugu Wananchi,
Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni moja ya changamoto za hifadhi ya Mazingira inayotishia uzalishaji wa chakula, ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi duniani kote. Hivyo, maadhimisho haya yanahimiza kuwepo kwa uwiano mzuri wa njia za uzalishaji, aina ya mazao yanayozalishwa na tabia ya ulaji ili kuepuka uharibifu wa ardhi na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.  Aidha, Kauli mbiu hii inalenga kukuza uelewa na kuhamasisha jamii kubadili mazoea ya kufanya shughuli za uzalishaji na matumizi ya rasilimali yasiyo endelevu kama vile, kufyeka misitu na kuchoma moto hovyo maeneo makubwa kwa ajili ya kupata ardhi ya kilimo na hivyo kuchangia uharibifu wa ardhi na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

Ndugu Wananchi,
Umuhimu wa kuadhimisha siku hii pamoja na mambo mengine umezingatia matokeo ya taarifa za tafiti mbalimbali duniani. Tafiti hizi zinaonyesha kuwa asilimia ishirini na tatu (23%) ya ardhi yote duniani haina uwezo wa kuzalisha. Aidha, asilimia sabini na tano (75%) ya ardhi yote duniani imebadilishwa kutoka kwenye hali yake ya asili na kuwa kwenye matumizi mengine ya ardhi hasa kilimo. Tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame imebaini kuwa ifikapo mwaka 2030, uzalishaji wa chakula cha kukidhi ongezeko la idadi ya watu duniani utahitaji hekta milioni mia tatu (300Ha) zaidi. Tathmini hii, inaonyesha kuwa mahitaji ya malighafi za kuzalisha nguo na viatu yanachangia asilimia nane (8%) ya uzalishaji wa gesijoto duniani ambapo yanatarajiwa kuongezeka kwa takribani asilimia hamsini (50%) ifikapo mwaka 2030.

Ndugu Wananchi,
Tangu mwaka 1994 nchi zilizoridhia Mkataba huu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa yasiyokuwa ya Kiserikali pamoja na wadau wengine, huadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazohusu kupambana na tatizo la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame. Maadhimisho ya siku hii yameendelea kuwa fursa muhimu katika kuhamasisha jamii kuchukua hatua katika ngazi zote ili kujenga ushawishi wa kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kwa nchi wanachama na Dunia nzima.

Ndugu Wananchi,
Ili kukuza uelewa wa jamii na kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana katika masuala ya hifadhi ya mazingira hususan kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameandaa shindano la kuandika Insha kuhusu hifadhi ya mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vijana wa vyuo vya elimu ya juu. Lengo la shindano hili ni kuelimisha kizazi cha sasa kuhusu Mazingira hususan Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, Mabadiliko ya tabianchi, pamoja na Hifadhi ya Bioanuai, hapa nchini.

Ndugu Wananchi,
Suala la matumizi bora na endelevu ya ardhi ni muhimu katika kupambana na kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, kwani kasi ya uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji inaongezeka kutokana na ukataji wa miti hovyo, ufugaji holela, kilimo cha kuhamahama, uchimbaji madini holela, uendelezaji wa makazi holela na kutokuzingatia maelekezo ya wataalam kunazidisha ukubwa wa tatizo hili. Kutokana na changamoto hizo, pamekuwepo na ongezeko la ukame, upungufu wa mazao ya chakula na biashara pamoja na kuongezeka kwa hali ya umaskini miongoni mwa jamii za watanzania.

Ndugu Wananchi,
Mnatambua kwamba nchi yetu ina uhitaji mkubwa wa ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kuzalisha chakula na uendelezaji wa shughuli za ufugaji kutokana na ongezeko la idadi ya watu. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia sitini na moja (61%) ya ardhi ipo katika hatari ya kugeuka jangwa na asilimia kumi na sita (16%) ya nchi nzima imekwisha onyesha dalili za wazi za kuwa jangwa. Aidha, utegemezi mkubwa wa rasilimali kama misitu umechangia kwa kiasi kikubwa katika tatizo. Tafiti zinaonyesha kuwa, asilimia themanini na tano (85%) ya watanzania wanategemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia. Utegemezi huu husababisha upotevu wa hekta mia tatu sabini na mbili elfu (372,000Ha) za misitu kila mwaka.  

Ndugu Wananchi,
Juhudi nyingi zimefanyika ili kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame hapa nchini. Juhudi hizo ni pamoja na, programu maalumu ya Mpango wa Kudhibiti Ukame (2018) ambapo utafiti wa kubainisha maeneo kame umeanza kufanyika nchi nzima; Sheria, Kanuni, Miongozo, Programu na Matamko mbalimbali kwa kuzingatia sekta ambazo zina utegemezi wa moja kwa moja na ardhi.

Mipango na Mikakati mingine ni kama Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji, 2006, ambao unatekelezwa katika mikoa yote Tanzania bara. Moja ya  maelekezo ya mkakati huu ni kupanda miti milioni moja na nusu(1,500,000) kila mwaka kwa kila halmashauri; Programu ya Pili ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II 2017/18 - 2028/29) ambayo inatekelezwa nchi nzima; Uanzishwaji wa Mashamba mapya ya Miti ambapo jumla ya hekta elfu moja mia saba na thelathini na nne (1,734) zimepandwa katika mashamba mapya ya miti ya Wino (Songea), Iyondo Msimwa (Ileje), Biharamulo (Chato), Mpepo (Mbinga), Buhigwe (Kigoma) na Mtibwa/Pagale (Mvomero). Aidha, shamba jipya kwa ajili ya uzalishaji wa gundi inayotokana na miti ya migunga lenye ukubwa wa hekta 50,000 limeanzishwa katika Wilaya ya Iramba (Singida).

Juhudi nyingine ni kuwepo kwa Mpango wa Mfumo wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (2013 – 2033) ambao unatekelezwa katika mikoa yote Tanzania bara; uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Mbadala wa Mkaa na Kuni ambapo majeshi, shule, vyuo, hospitali, na baadhi ya hoteli za kitalii hapa nchini  zinatumia nishati mbadala wa mkaa; uhamasishaji wa usimamizi Shirikishi wa Misitu ambapo jamii zinashiriki kulinda na kuhifadhi misitu na hivyo kunufaika na misitu hiyo.  

Ndugu Wananchi,
Pamoja na utekelezaji wa Sheria, Mipango na Mikakati mbalimbali ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame hapa nchini, Serikali imeelekeza jamii kuongeza juhudi katika utekelezaji wa mipango na mikakati hiyo. Maelekezo haya ni pamoja na kuendeleza kampeni ya upandaji miti milioni moja na nusu (1,500,000) kila mwaka kwa kila Halmashauri, kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame ambapo kila sekta imepewa jukumu la kuutekeleza na kuhuisha Mpango huu katika Mipango yao ya Kisekta; kuendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu kupambana na kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame pamoja na athari zake; kusimamia na kutekeleza Kanuni bora za Matumizi endelevu ya Ardhi zilizoelekezwa kwenye Mpango wa Kitaifa wa Matumizi ya Ardhi.

Ndugu Wananchi,
Katika kupunguza utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa ambayo husababisha ukame na kuenea kwa jangwa, Serikali, ipo katika ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere Hydropower Station lenye uwezo wa kuzalisha megawati za umeme zaidi ya elfu mbili mia moja kumi na tano (2,115MW). Umeme huu utapatikana kwa bei rahisi na hivyo kuwezesha wananchi wa kawaida na taasisi kutumia umeme kama nishati ya kupikia. Sambamba na hilo serikali inaendelea na ujenzi wa reli kwa ajili ya treni ya umeme (Tanzania Stardard Gauge Railway-SGR) kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara zetu na hivyo, kupunguza uzalishaji wa gesijoto unaosababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huchangia kuwepo kwa hali ya jangwa na ukame.

Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka kuwa mwaka 2018 Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Kampeni ya kuifanya Dodoma iwe ya kijani na kuelekeza Kampeni hii itekelezwe mikoa yote. Lengo la kampeni hii ni kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi katika jiji la Dodoma kwa kupanda na kutunza miti. Katika kampeni hii jumla ya miti milioni moja mia nne na mbili elfu mia nane kumi na mbili (1,402,812) ilipandwa kati ya mwaka 2018 hadi 2020 katika ukubwa wa hekta elfu tatu mia tano na saba nukta mbili (3,507.2Ha) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma na kati ya miti hiyo asilimia themanini na moja nukta saba tatu (81.73%) inafanya vizuri. Aidha, mafanikio ya Kampeni hii ni chachu ya kuendeleza shughuli za upandaji miti katika mikoa mbalimbali hapa nchini na hivyo kuchochea juhudi za Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.

Ndugu Wananchi,
Ili kutekeleza kampeni ya Mhe. Makamu wa Rais, kwa kipindi cha mwaka 2018/19 nchi yetu iliweka malengo ya kupanda miti milioni mia tatu kumi na tatu mia moja tisini na sita elfu mia tano (313,196,500) katika mikoa yote. Ili kufanikisha lengo hili, kiasi cha miti iliyopandwa ni milioni mia mbili na tisa miasaba sitini na saba elfu mia nane kumi na tano ( 209,767,815) ikiwa ni asilimia sabini na mbili nukta sita (72.6%) ya lengo zima. Kati ya miti yote iliyopandwa, iliyopona ni miti milioni mia moja hamsini na tatu, mia mbili themanini na nane elfu, mia nane arobaini na tano (153,288,845) sawa asilimia sabini na tatu nukta moja (73.1%) ya miti yote iliyopandwa. Hali hii inaonyesha kuwa wananchi wanafanya juhudi kubwa katika kukabiliana na hali ya jangwa na ukame kwa njia ya kupanda na kutunza miti. 

Ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wadau wote wa Mazingira walioshirikiana na Serikali kuandaa na kusimamia program mbalimbali za kupambana na hali ya ukame na kuenea kwa jangwa hapa nchini. kwa madhumuni ya kudhibiti kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula na malighafi ili tukabiliane na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

Kwa namna ya pekee navishukuru vyombo vya habari kwa kufanya jitihada za kuelimisha umma juu ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame nchini.
Asanteni kwa Kunisikiliza.
MUSSA AZZAN ZUNGU (MB)
WAZIRI WA NCHI – OFISI YA MAKAMU WA RAIS
MUUNGANO NA MAZINGIRA
17 JUNI, 2020