IMEFAHAMIKA kuwa, Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ametumia Sh Mil 60 kusajili viungo wawili, Mzamiru Yassin na Said Ndemla kuendelea kusalia klabuni hapo.

Viungo hao ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ambao wote wamesaini miaka miwili.

Taarifa zinaeleza kuwa viungo hao kila mmoja amesaini mkataba wa miaka miwili na kuchukua Sh Mil 30, hivyo kwa wawili jumla ni Sh Mil 60.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wachezaji hao wamesaini mikataba hiyo baada ya kufikia muafaka mzuri na viongozi wa timu hiyo na mameneja wanaowasimamia.

“Kama kuna mchezaji wa Simba ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu na hajafanya mazungumzo yoyote na viongozi, basi huyo hayupo kwenye mipango ya kocha.

“Tayari baadhi ya wachezaji wameanza mazungumzo na viongozi na kati yao wapo waliosaini mikataba akiwemo Mzamiru na Ndemla ambao wote wawili wamesaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh Mil 60 kwa kila mmoja kuchukua Sh Mil 30,” alisema mtoa taarifa huyo.

Hivi karibuni, Mo alitamka kuwa: “Hakuna mchezaji yeyote aliyekuwa kwenye mipango na kocha tutakayemruhusu kuondoka Simba, wachezaji wote waliopo katika mipango ya kocha watabaki kwa gharama yoyote.”