SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya corona, ambapo hadi sasa wapo wagonjwa 10 tu wanaopata huduma za afya katika vituo vilivyopo Unguja na Pemba. Vituo vinne vimefungwa baada ya kukosa wagonjwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed alisema hayo wakati akiwasilisha Makadirio, Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2020/2011, Chukwani, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema hadi sasa wapo wagonjwa 10 waliolazwa katika vituo vinavyotoa huduma za wagonjwa hao. Alisema Pemba yupo mgonjwa mmoja katika kituo kiitwacho Vitongoji. Aliongeza kuwa baadhi ya vituo vilivyokuwa vikitoa huduma za wagonjwa hao, tayari vimefungwa baada ya kukosa wagonjwa wa aina hiyo.

Spika napenda kulijulisha Baraza la Wawakilishi kwamba tumepata mafanikio makubwa katika kudhibiti na kupambana na ugonjwa wa corona, ambapo kwa sasa wapo wagonjwa 10 wanaopata matibabu katika vituo vinavyopokea wagonjwa hao Unguja wakati kwa upande wa kisiwa cha Pemba yupo mgonjwa mmoja,”alisema.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na mwongozo na maelekezo, yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wakuu wa nchi, Rais Dk John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ikiwemo kuwatoa hofu na wasiwasi wananchi kuhusu ugonjwa huo.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kufuata masharti ya afya katika kujikinga na virusi wa corona, ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na sababu, kuvaa barakoa na kusafisha mikono kwa kutumia vitakasa mikono.

Alisema serikali itaendelea kulegeza masharti yaliyowekwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo hatua kwa hatua katika siku za hivi karibuni. Tayari serikali imetoa ruhusu kufunguliwa kwa vyuo vikuu na kidato cha sita kwa ajili ya matayarisho ya mitihani ya taifa.

“Hali ni nzuri, tunaweza kuruhusu baadhi ya mashirika ya ndege kuja nchini kwa ajili ya kuleta watalii hivi karibuni,” alisema.

The post Serikali ya Zanzibar yaidhibiti Covid-19 , wagonjwa wabaki 10 tu appeared first on Bongo5.com.