Serikali imewaahidi wafanyabiashara wa minofu ya samaki kuongeza idadi ya mashirika ya ndege yatakayosafirisha mzigo huo ili kuwafikia walaji kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati wa kikao cha pili kilichowakutanisha Mawaziri wa Wizara tano zikiwemo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Mambo ya Nje ya Nchi, Viwanda na Biashara, Fedha na Mipango na Kilimo.

“Mpaka sasa kuna mashirika zaidi ya mawili ambayo tunafanya mazungumzo nao ili kuleta ndege mkoani Mwanza, hivyo changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza usafirishaji huo zinaendelea kushughulikiwa’, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Mhandisi Kamwelwe, amesema baadhi ya changamoto ambazo zimeshashughulikiwa mpaka sasa ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa uzio na maboresho ya jengo la kutunzia mizigo.

Aidha, Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema pamoja na jitihada hizo Wizara kupitia kamati iliyoundwa inaendelea kutafuta masoko ya samaki ili kufikia lengo la kusafirisha tani zaidi ya 100 kwa safari moja.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina, amesema pamoja na mzigo wa samaki na mabondo tayari uzalishaji wa bidhaa za nyama umeanza na wizara imejipanga kuhakikisha mzigo huo unasafirishwa nje ya nchi ili kuongeza pato la Taifa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo mkoani Mwanza.

“Kwa Mkoa wa Mwanza peke yake uzalishaji wa nyama umeanza na matarajio ni kusafirisha zaidi ya tani hamsini kwa safari moja, kama Wizara tumejipanga vizuri kwenye jambo hili na huo ni mwanzo tu”, mesema Mpina.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongela ameishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zilizojitokeza na kuahidi kuendelea kuhamasisha viwanda kuzalisha zaidi ili kuongeza pato na kuongeza ajira kwa wanaMwanza.

Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema toka kuanza kwa usafirishaji huo mapema Aprili 22, mwaka huu, mpaka sasa tani zaidi ya 140 zimeshasafirishiwa ambapo mpango ni kusafirisha zaidi ya tani 100 kwa safari moja.