Spika wa Bunge, Job Ndugai ametoa ya moyoni kuhusu hatua ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake kuwania urais, kwa kile alichodai kuwa hana sifa za kutosha.

Akizungumza katika mahojiano maalum na chombo kimojawapo cha habari nchini, Spika Ndugai amesema kuwa licha ya kuwa ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni lakini anapungiwa sifa muhimu kupewa nafasi ya urais.

Akitolea mfano wa sakata lilidaiwa kuwa ni la kushambuliwa kwa kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani bungeni, Spika Ndugai alidai kushangazwa na kile alichodai kuwa ni uongo wa kusingizia kushambuliwa jambo alilosema kuwa halikuwa la kweli bali kiongozi huyo alikuwa amelewa.

“Kwanini usiseme tu kuwa nilipiga kinywaji kidogo watu wakuelewe, lakini mpaka usingizie kwamba watu wamekula njama na nini ,na hawa ndio watu wanaojaza fomu eti wanataka urais ha ha ha na vyombo vya habari hata haviulizi kuwa hata wewe” amesema Spika Ndugai  na kuongeza kuwa;

“Nilimkuta hana scratch (mkwaruzo) yoyote, nilichokuta ni ule mguu ukiwa na ‘clip bandage’ na vitu vya namna hiyo” amesema Spika Ndugai

Spika Ndugai aliendelea kusisitiza madai kuwa Mwenyekiti huyo wa Chadema hakushambuliwa bali alikuwa amelewa jambo ambalo vyama vya upinzani na hasa Chadema yenyewe vimelipinga vikali huku wakitoa mfano wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki ambaye naye alishambuliwa na watu wasiojulikana Jijini Dodoma.

Alipoulizwa kuhusu hali ya demokrasia katika bunge aliloliongoza na kile kinachoonekana kuwa ni kubanwa kwa wabunge wa upinzani Spika Ndugai aliwatupia lawama baadhi ya wabunge ambao hata hivyo hakuwataja majina kuwa wanatumia madawa ya kulevya na kuvuta bangi.

“Ni ukweli usiopingika kwamba yako mambo Watanzania hawayajui na huwa hatupendi sana kusema ni kweli baadhi ya wabunge na hasa hao wenye fujo baadhi yao wanatumia madawa ya kulevya, wanatumia bangi, baadhi yao wanakunywa konyagi au gongo gani, wanakuja pale sio yeye

“Tulifika mahali ambapo tumewafungia wabunge wengine mwaka mzima asirudi bungeni, mbunge mwingine mnampeleka kwenye kamati ya maadili anaenda anawaambia mimi nimefanya na nikipata nafasi narudia tena na msinisamehe na viadhabu vyenyewe kwenye vitabu ni vidogo

“Nitumie nafasi hii kuwaomba vyombo vya habari, tumekuwa tukikuza watu wa hovyo, waropokaji ndio wanakuzwa kuonekana ni heroes. Bahati nzuri naamini wapiga kura watawachuja watu wengi katika hawa maana hamna walichokifanya jimboni”

“Hakuna ambalo sikufanya kumsaidia Tundu Lissu siku ya tukio nilikuwa Dar nilipotua Dodoma nikaenda Hospitali tuka-mobilize madaktari waliokuwepo Mhe Mbowe na wenzake wakasema si kweli kwamba hawaamini Muhimbili bali ili wapate amani ya moyo wanaomba wampeleke Nairobi

“Sijawahi kuongea na Tundu Lissu kwa simu kwa sababu namjua namfahamu vizuri ni mtu ana imani zake fulani na mapambano, ana ruti yake anayoiendea ambayo yeye ndio anaweza kuielewa vizuri zaidi na anaona sisi wengine ni mashetani, mtu aina hiyo unampa amani, unamuacha

“Bunge la 9 wakati wa kina Mzee Slaa palikuwa na wapinzani ambao walikuwa wakifanya kazi yao, walikuwa wanashusha hoja ambazo tukikaa pembeni kama CCM tunaambiana kuwa tunaharibiana” - Mhe Ndugai