Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt Magufuli amewataka wanachama wote wa chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha kugombea nafasi wanazoomba.

Mwenyekiti huyo amesema hayo alipokuwa akikagua kumbi za Kituo cha Mikutano Dodoma (Jakaya Kikwete Hall) ambako utafanyika Mkutano Mkuu wa CCM, na amesisitiza kauli yake aliyowahi kuitoa kuwa uchaguzi mkuu upo pale pale.

“Chama chetu kinayo demokrasia ya kutosha, lakini demokrasia hii ndani ya chama isije ikatumika kuleta fujo, kutugombanisha na kukiumiza chama, tuweke maslahi ya chama mbele na tutumie nafasi hii kukiimarisha chama chetu,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amewataka wana CCM kote nchini kutembea kifua mbele na kuyasema mambo yote ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wananchi, badala ya kuacha jukumu hilo kwa viongozi wachache.