BERNARD Morrison kiungo mshambuliaji wa Yanga amesema kuwa alifuatwa na viongozi wa Simba ambao walikuwa wakimshawishi kumpa mkataba ili atue ndani ya klabu yao.

Morrison kwa sasa anakipiga ndani ya Yanga amekuwa akihusishwa kujiunga na Simba baada ya uongozi wa Simba kuvutiwa na uwezo wa kiungo huyo mwenye madoido kwenye kumiliki na kucheza na mpira uwanjani

Hakuwa kwenye sehemu ya mchezo dhidi ya Mwadui FC uliochezwa Juni 13 kwa kudai kuwa bado alikuwa hajawa fiti.

Kuhusu mkwanja wa Simba amesema:- "Simba walinifuata nikawaambia wanipe ofa yao, wakanipa. Lakini baadaye wakaleta dola 10,000 walisema zimetoka kwa Rais wa Simba ikiwa ni sehemu ya kunishawishi nisaini kwao.

 " Nilitakiwa nichukue dola 5,000 na 5,000 achukue yule wakala. Mwisho nikasema sawa, nitachukua lakini kuhusiana na kusaini mkataba wao nitafikiria kwanza, lakini baadaye naona imekuwa shida na yule wakala ananisumbua sana, kwamba nimechukua fedha ya Simba nitakuwa matatizoni, lakini walinipa wenyewe na haihusiani na suala la kusaini mkataba," amesema.

Morrison amefunga mabao matatu ndani ya ligi akiwa amecheza mechi 10 na ametoa pasi tatu za mabao pia.