Morrison Agomea Safari ya Shinyanga

WAKATI ishu ya David Molinga kudaiwa kugoma kuambatana na timu kwenda, Shinyanga kwa mchezo dhidi ya Mwadui, Juni 13, imebainika kuwa, hata winga machachari wa Yanga, Bernard Morrison hajasafiri na wenzake kwenda huko kwa sababu ambazo hazijafahamika. 
Yanga inatarajia kucheza na Mwadui FC siku ya Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye uwanja wa CCM Kambarage ukiwa ni wa kwanza tangu ligi iliposimama Machi 17 kutokana na tatizo la kusambaa kwa virusi vya Corona.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema, Morrison hakuwepo kwenye basi la timu wakati linaondoka na hakukuwa na taarifa zozote za kukosekana kwake pamoja na kujumuishwa kwenye orodha ya wachezaji waliotakiwa kusafiri.

Mkwasa alisema kuwa meneja wa timu hiyo, Abeid Mziba alifanya juhudi za kumpigia simu, lakini ilishindikana na waliamua kuondoa gari baada ya kusubiri kwa muda.

“Sina taarifa zozote kuhusiana na kutosafiri kwa Morrison. Tulifanya kila jitihada, hazikufanikiwa, hivyo labda uongozi wana taarifa zake. Kwa sasa tunakaribia Dodoma,” alisema Mkwasa kwa njia ya simu.

Mkwasa alisema kuwa mchezaji mwingine ambaye hajasafiri ni kipa Metacha Mnata ambaye mke wake amejifungua na Papy Tshishimbi na Mohamed Issa 'Banka' ambao ni wagonjwa.
Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alikiri kukosekana kwa Morrison katika msafara huo.

“Mimi nipo kwenye gari hili la wachezaji naelekea Shinyanga, ni kweli kuwa Morrison alijumuishwa na hayupo kwenye huu msafara. Sijui kuna shida gani, lakini mipango inafanyika kumfanya yeye, kipa Metacha na Kocha Mkuu, Luc Eymael wanakuja Shinyanga kabla ya mechi,” alisema Bumbuli.

Awali ilielezwa straika anayongoza kwa mabao ndani ya Yanga, Molinga aligoma kuambatana na timu licha ya kufuatwa nyumbani kwake asubuhi ya leo, japo mwenyewe amesema hakuwepo kwenye orodha ya wanaosafiri iliyotangazwa na Msemaji wa klabu, Hassan Bumbuli.