UONGOZI wa Klabu ya Yanga wakishirikiana na wadhamini wao Kampuni ya GSM Mei 31 wameingia mkataba wa misimu minne wa makubaliano ya kimaendeleo ya timu hiyo na kampuni La Liga ambao utagharimu kiasi cha euro 1,040,000, sawa na shilingi bilioni 2.6 za Kitanzania.

Makubaliano ya kuingia mkataba huo yalifikiwa kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar ambayo yatahusisha maendeleo ya mchezo wa soka nchini kupitia La Liga ambayo yanahusisha masuala ya ufundi na vifaa mbalimbali.

Maelezo ya mkataba huo ulio na vipengele vinne, vinaitaka Yanga na GSM kuilipa La Liga fedha hizo katika awamu nne tofauti kuanzia msimu wa 2019-20 hadi msimu wa 2022-23.

Malipo ya kwanza ya mkataba huo yanatarajiwa kufanyika kati ya kipindi walichoingia mkataba huo hadi Agosti 31, mwaka huu kwa Yanga na GSM kuilipa La Liga kiasi cha euro elfu 80 ambayo ni sawa na Sh milioni 204 baada ya makato iwapo yatatokea.

Wakati malipo ya pili ambayo yatafanyika msimu ujao katika kipindi kati ya Septemba mwaka 2020 hadi Juni 2021, yatakuwa ni kiasi cha euro 360,000, sawa na Sh milioni 918

Katika msimu wa tatu ambao malipo yake yanatakiwa kufanyika katika kipindi cha kuanzia Julai Mosi, 2021 hadi June 30, 2022, Yanga na GSM watalipa jumla ya kiasi cha euro 300,000 ambayo sawa na Sh milioni 765, kiasi ambacho ni sawa na kitakacholipwa kwenye msimu wa mwisho kwenye mkataba huo.

Kazi kubwa ya La Liga kwa mujibu wa mkataba huo itakuwa ni kuhakikisha wanasaidia maendeleo katika soka la kisasa Yanga huku wakiongeza thamani ya timu hiyo nchini.Watakuwa wakitoa huduma na wataalamu kwa ajili ya kuwaelekeza Yanga, namna ya kuendesha soka la kisasa.

Mkataba huo umeweka wazi Yanga na GSM wana haki ya kuvunja makubaliano hayo kwa kutoa taarifa ya maandishi ambayo itakuwa inaeleza sababu ya kutaka kuvunja mkataba huo ikiwa itatokea uvunjifu wa makubaliano ya mkataba wao.

Chanzo: