*Asema anasumbuliwa na marafiki zake, wanamuuliza nani baada ya Magufuli?


MBUNGE wa Jimbo la Nkasi Ally Kessy(CCM) ameliambia Bunge kuwa kuna kila sababu ya Rais Dk. John Magufuli aongezewe muda wa kuwa Rais huku akisisitiza kuwa Rais atake au asitake lazima aongeze muda.

Amesema yeye(Kessy) amekuwa akipata tabu sana kwani amekuwa akiulizwa na marafiki zake wa ndani na nje ya nchi kwamba baada ya Magufuli nani anafuata lakini jibu lake analowajibu ni kwamba Rais ataongeza muda.

Akichangia Bungeni Mjini Dodoma , leo Juni 9,2020 wakati akichangia Azimio la kumpongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyosimama mara katika mapambano dhidi ya Corona, Kessy amesema kuwa kutokana na janga la Corona hata zilikoanzia dini Italia na Saud Arabia walifunga Misikiti na Makanisa.

&ot;Watu wanatetemeka, akabaki mwanaume mmoja tu jasiri peke yake anaitwa Magufuli. Sasa mheshimiwa Rais mimi napata tabu sana.Nina marafiki sehemu mbalimbali, wananiuliza baada ya Magufuli nani anayefuata katika nchi yenu?

"Leteni rasimu ya kuongeza muda akitaka asitake , maana alipotufikisha hapa mheshimiwa Rais ni pazuri, labda nyie hamsumbuliwi sumbuliwe, Dunia zima ni mfano ametoa, kuna nchi nyingine watu wamepigwa kwa ajili ya Corona, watu wameuawa, watu mmesikia na mmeona kwenye matelevisheni , watu wanafuatwa makanisani na misikiti wanapigwa tu viboko.

"Wamekufa kwa njaa watu, Rais wetu msimamo wake huu Mwenyezi Mungu amsimamie na amuongoze, lazima tumpongeze kwa hali ya juu .Ila sasa kuna watu wengine wanafiki, wanafiki, wanafiki tunao.

"Katiba mheshimiwa sio Msahafu , sio Msahafu Katiba, Katiba inabadilishwe na anakuwa sio Rais wa kwanza kuongezewa muda , alazimishe atake asitake, alazimishwe .Haiwezekani kumuachia nafasi anasema amekataa , amekataa kwa vipi ? alazimishe tu,"amesema Kessy.

Amesisitiza Rais Magufuli kitendo alichofanya tu kwenye Corona amekuwa mfano wa kuigwa, Dunia zima kila mtu wanamsapoti."Napata shida labda ninyi amsumbuliwi, huenda hamna marafiki duniani na huko kwenye nchi nyingine.

"Lakini mimi napigiwa simu kila siku naulizwa baada ya Magufuli nani?Nakosa jibu. Mimi jibu langu nasema anaongoza muda ,ataongeza muda akitaka asitake , tutapiga kura.

"Mimi nimemsikia dada yangu tena wa CUF amezungumza kwa uchungu sana hapa na kweli Rholida, kwa kweli amechangia vizuri, amekuja baba Paroko(Joseph Selasini), tunamuamini sana tena ni mpinzani , sasa amebaki nani wa kusema sema hapa hakuna, Rholida kamaliza, Baba Paroko kamaliza , Lijualikali kaja kuwachinja.

"Lakini sasa inafuata nini hapa baada ya kupongeza, tutakuwa tunapongeza ...tunapongeza kila baada ya miaka mitano , Rais Magufuli aendelee tu, Katiba sio Msahafu tupige kura na hiyo Oktoba tupige kura ya kumchagua na hapo hapo kumtaka Rais aongeze muda,"amesema Kessy.

Ameongeza kwanza haitakuwa gharama mara mbili kwani mwananchi anapiga kura ya kumchagua kwenye uchaguzi mkuu na kisha anapiga na kura ya Rais aongezewe muda au asiongezewe muda.

"Rais pekee kusema mimi sitaki tunamlazimisha , tuna viongozi wa kwenda kumlazimisha kwa nguvu. Tutengue hicho kipengele, haiwezekani kwenye janga kama hili Dunia zima inateseka lakini Rais wetu alikuwa na msimamo wa hali ya juu... haiwezekani.

"Haijatokea , tusiwe wanafiki haijatokea, nchi nyingine watu wameuawa kwasababu ya Corona hii, watu wanapigwa kwa Corona hii, watu wamekufa njaa kwa Corona hii lakini Rais wetu amekuwa na msimamo wa ajabu kabisa .

"Haiwezani , Mwenyezi Mungu amemuongoza kwa hali ya juu kabisa, kwanini tusimuombe, yeye amekuwa nani tusimuombe akaongoza muda? Asitusikie sisi wananchi wake kwa vipi? Kwa hiyo tunamuomba lazima aongeze muda akitaka asitake, sisi tunamuomba.Hakuna mjadala katika hili,"amesema Kessy.

Wakati Kessy akitoa mchango huo, Spika wa Bunge Job Ndugai alimkatisha na kumuomba hilo analosema aliweke moyoni na baada ya uchaguzi mkuu kumalika na kisha wakarudi Bungeni hilo suala linajadilika kwani liko ndani ya uwezo wao wabunge.