Makumi ya maelfu ya wananchi wa Mali wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu Bamako, wakishinikiza kujiuzulu Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamesikika wakilaani uongozi mbaya na kashfa za ufisadi zinaoikabili serikali ya Rais Keita.

Katika maandamano hayo ya jana Ijumaa, Cheick Oumar Sissoko, kiongozi wa upinzani nchini humo amewaambia wafuasi wake walioshiriki maandamano hayo kuwa, "tumeafikiana kuunganisha nguvu na kambi zetu zote hadi pale rais atakapojiuzulu."

Keita ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Mali kwa muhula wa pili mwaka 2018, anaandamwa na ukosoaji mkubwa kwa kushindwa kuimarisha usalama eneo la kaskazini mwa nchi, kufeli kuipatia ufumbuzi migomo ya walimu, kushindwa kulishughulikia janga la corona na mvutano wa kisiasa uliosababaishwa na uchaguzi tata wa bunge wa mwezi Machi mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa, Mali imekuwa katika mivutano ya kisiasa tangu kuibuka machafuko nchini humo mwaka 2012 yaliyosababisha uasi wa baadhi ya wanajeshi na kumpindua Rais Amadou Toumani Toure ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa muda kwa miaka 10.