Korea Kusini imefanya mkutano wa usalama wa dharura leo na kuihimiza Korea Kaskazini kuzingatia makubaliano ya maridhiano, saa kadhaa baada ya Korea Kaskazini kutishia kubomoa ofisi ya uhusiano na kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya mpinzani wake. 

Katika taarifa kutoka ikulu ya rais , Mkurugenzi wa kitaifa wa masuala ya usalama wa Korea Kusini Chung Eui-yong, aliandaa mkutano wa dharura kwa njia ya video pamoja na waziri wa usalama na wakuu wa kijeshi kuzungumzia hali ya sasa katika rasi ya Korea na hatua ambazo huenda zikachukuliwa na serikali. 

Kuna wasiwasi kuwa Korea Kaskazini inaweza ikaanza kutumia uchochezi kuimarisha umoja wake wa ndani na kupinga makubaliano, huku mazungumzo ya nyuklia kati ya taifa hilo na Marekani yakikwama. 

Waangalizi wanasema Korea Kaskazini  inahitaji kwa haraka kulegezewa vikwazo, wakati ikikabiliana na janga la corona na vikwazo iliyowekewa na Marekani.