Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amefichua kuwa alilazimika kutumia usafiri wa lori la mizigo kutoka nchini kwao Romania hadi Ujerumani alikopandia ndege, kwa sababu kulikuwa hakuna magari au ndege zinazoruhusiwa kuingia kwao.

Cioaba pamoja na Kocha wa Viungo, Costel Birsan, wameshawasili nchini tokea juzi na ndege ya Shirika la Ethiopia, waliyopandia mjini Frankfurt, Ujerumani, ambapo tayari wameshaanza kukinoa kikosi cha Azam FC kinachojiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Cioaba alisema hadi wanafika Ujerumani walisafiri na lori hilo kwa takribani saa 23 njiani, wakidanganya kuwa ni madereva wasaidizi, wakikatisha katika nchi za Hungary na Austria kabla ya kuingia Ujerumani.

“Nilijaribu kabla kwa muda mrefu kutafuta tiketi lakini ilikuwa ngumu kwa kuwa nchi yangu bado hadi sasa usafiri wa ndege haujaanza wamefunga uwanja wa ndege, lakini nilisubiri fursa nyingine kabla ya wiki moja kupita tukapewa ruhusa ya kusafiri na gari, nikaondoka na gari haikuwa rahisi tulisafiri saa 23, kwa sababu tulitoka Romania hadi Hungary saa nane, Hungary hadi Austria saa nane, Austria hadi Ujerumani saa zingine nane au tisa,” alisema.

Alisema aliamua kujitoa muhanga na kusafiri kwa njia hiyo kwa sababu ya kuipenda kazi yake, akitaka kuwahi kurejea ili kukaa pamoja na timu yake na kuendeleza malengo waliyojiwekea, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dr. John Magufuli kwa kuruhusu watu kuingia nchini.

“Asante kwa Rais wa Tanzania kwa kuwapa watu nafasi ya kuingia nchini na kuanza kazi, kwa sababu asingefungua Uwanja wa Ndege (usafiri wa ndege kimataifa), ingekuwa ni vigumu kuja na pia namshukuru kwa kutoa nafasi kwa timu zote za mpira kuanza mazoezi na kucheza tena kwa sababu haya ndio maisha yetu,” alisema.

Kocha huyo bora wa ligi mwezi Novemba na Januari msimu huu, pia aliushukuru uongozi wa Azam FC kwa kuendelea kuisadia timu hiyo kwa kipindi hiki kigumu cha miezi miwili baada ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).

Robo fainali ASFC  

Baada ya Azam FC kupangwa na Simba kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), Cioaba alisema anaiheshimu Simba lakini atakipanga kikosi chake kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

“Ni mechi ya tofauti, kwenye ligi ni ligi na kwenye Kombe la FA ni mechi tofauti inahitaji umakini mkubwakwa mechi hiyo, napenda kongelea mechi hizi mbili (za ligi) dhidi ya Simba, naiheshimu Simba hivi sasa ipo nafasi ya kwanza inacheza mpira mzuri lakini usisahau mechi ya mwisho niliyopoteza 3-2 ilikuwa mechi moja nzuri na goli la Simba lile la tatu mpira ulikuwa umetoka na mwamuzi aliwapa nafasi ya kushinda, lakini naisheshimu Simba na hali ndio iko hivyo,” alisema.

The post Kocha Azam FC asafiri kwa Lori la mizigo kuja Tanzania akitokea Romania, atumia saa 23 kufika Ujerumani appeared first on Bongo5.com.