HATIMAYE kiungo anayehusishwa kujiunga na Yanga, Fabrice Mugheni, amewaaga rasmi mashabiki wa timu yake ya Rayon Sports ya Rwanda kuwa anaondoka mwishoni mwa msimu huu. Fabrice aliwahi kusema kuwa aliombwa video zake na Injinia Hersi Said ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM ambaye pia anahusika na masuala ya usajili ndani ya Yanga.

Fabrice kupitia mtandao wake wa Instagram, aliwaaga rasmi mashabiki wa timu hiyo jambo ambalo linatafsiriwa kama huenda akawa alishamalizana na Yanga kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, kiungo huyo alisema kuwa ni kweli ataondoka mwishoni mwa msimu huu, ndiyo maana ameamua kuwaaga rasmi mashabiki wa timu yake ili wakiona lolote wasishangae japo hakutaka kuweka wazi ni sehemu gani atakwenda.“Nimeamua kuwaaga mashabiki wa timu yangu ili wakiona chochote wasiwe na maswali mengi ya kujiuliza kichwani, hii inatokana na mimi kuondoka ndani ya Rayon mwishoni mwa msimu huu.

 

“Haitakuwa rahisi mimi kusema wapi nitaelekea ila kwa kuwa mpaka nimeaga basi fahamu kuwa nitaondoka mwishoni mwa msimu huu mpaka pale mambo yatakapokuwa kamili watu watafahamu kuwa nimehamia wapi,” alisema mchezaji huyo.

 

Alipotafutwa Injinia Hersi Said kufunguka juu ya suala la Fabrice Mugheni, alisema: “Kwa sasa kama uongozi unajitahidi kuhakikisha timu inafanya vizuri katika maandalizi ya ligi, hivyo masuala yote ya usajili ukifika muda wake kila kitu kitakuwa wazi.”

 

Kama akitua Jangwani, basi kiungo huyo atapokelewa kwa heshima kama ambavyo wamekuwa wakipokelewa wachezaji wengine wapya wanapotua Yanga.

 

Yanga imedhamiria kufanya usajili makini na babkubwa kwa ajili ya kutawala soka la Bongo kuanzia msimu ujao, ikiwa chini ya udhamini wa kampuni ya GSM ambayo imedhamiria kuifanya timu hiyo itambe kitaifa na kimataifa.