Kiongozi wa upinzani nchini Malawi Lazarus Chakwera ameshinda duru ya pili ya uchguzi wa urais, maafisa wanasema.

Alimshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika kwa asilimia 58.57 ya kura katika uchaguzi wa Jumanne, tume ya uchaguzi ilitangaza usiku wa Jumamosi.

Mwezi Februari, Mahakama ya katiba nchini Malawi ilifutilia mbali ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa Mei 2019, kutokana na dosari zilizokumba uchaguzi huo.

Nchi iligawanyika vikali wiki kadhaa kuelekea uchaguzi wa marudio.

Malawi ni nchi ya kwanza Afrika kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais na kuandaa duru ya pili ambayo upinzani ukanyakua ushinda.

Bw. Chakwera anatarajiwa kuapishwa leo Jumapili.

Kama ilivyotokea Malawi nchini Kenya upinzani ulipinga matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka 2017 na kushinda mahakamani.

Hata hivyo mgombea wa upinzani Raila Odinga alisusia duru ya pili ya uchaguzi.

Baada ya matokeo rasmi kutangazwa usiku wa Jumamosi, Bw. Chakwera alisema ushindi wake ni "ushindi wa demokrasia na haki" na kuongeze kusema: "Roho yangu imejaa furaha."

Wafuasi wake walimiminika katika barabara za mji mkuu wa Lilongwe, kushangilia ushindi wao baadhi wakipiga honi za magari na wengine wakipiga fataki.

Tukio hili lina umuhimu mkubwa katika historia ya siasa nchini Malawi, na linaonesha wadi kwamba mahatma na time ya uchaguzi hazikuwa tayari kushinikiza kufanya maamuzi kwa kwa maslahi ya ofisi ya rais.

Baada ya hatua hiyo Bw. Mutharika alikimbilia mahakama ya rufaa kupinga uamuzi huo lakini majaji walisimama kidete kutoa uamuzi usioegemea upande wowote.

Na sasa wananchi wamefanya uamuzi wao kwa kumemkataa katika duru ya pili ya uchaguzi.

Ushindi wa Peter Mutharika mwaka jana ulifutwa na mahakama ya katiba baada ya ushahidi kuonesha kuwa uchaguzi wa mwaka jana yalichakachuliwa.

Bwana Mutharika sasa analalamika kwamba uchaguzi huo haukuwa wa haki na huenda akawasilisha malalamishi yake mahakamani, lakini raia wa Malawi wamemchagua Lazarus Chakwera kama rais wao mpya.

Akizungumza kabla ya matokeo hayo ya Jumamosi, bwana Mutharika alisema kwamba licha ya kwamba matokeo ya uchaguzi huo ''hayakubaliki'' , ni ''matumaini kwamba raia wa taifa hilo watalisukuma mbele gurudumo la taifa hilo badala ya nyuma''.

Muhubiri huyo wa kanisa la Pentecostal na muhadhiri wa somo la theolojia atalazimika kuponya vidonda vya taifa ambalo limepitia miezi kadhaa ya msukosuko wa kisiasa.

Rais mteule, Lazarus Chakwera sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuleta nchi pamoja kufuatia mgawanyiko uliojitokeza na kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Pia ana kibarua cha kukabiliana na ufisadi, kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira, mambo amabayo yalikuwa ni miongoni mwa masuala ya msingi katika uchaguzi huo.