Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahaman Kinana, amemwomba msamaha hadharani Mwenyekiti wa CCM, Taifa, Dk. John Magufuli.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, alitangaza hadharani kuomba msamaha huo kwa makosa aliyoyatenda kipindi chake cha uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Kinana alisema akiwa kiongozi anaamini kuwa yapo mambo aliyoyafanya ambayo yaliwakwaza viongozi wengine akiwamo Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli, ambaye ni Rais wa Tanzania na anaamini atamsamehe.

“Naamini ilifika wakati nikakereka na kusema maneno ambayo yanaweza kuwa siyo mazuri, nimekaa na kutafakari sasa, namuomba radhi Mwenyekiti wa CCM, Magufuli,” alisema Kinana na kuongeza:

“Kama kiongozi ni kweli naamini ilifikia hatua nikatofautiana na wenzangu ama niliwakera wenzangu na pia, hata kiongozi wangu, Mwenyekiti wa Chama, kiukweli ninamwomba radhi.”

Akiwa Arusha, Kinana pia alikutana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zelote Steven na Katibu wa Mkoa wa huo, Mussa Matoroka na kuwaeleza kuwa pamoja na kustaafu, ataendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ndani na nje ya chama chake.

“Mimi kwa sasa nimestaafu uongozi, ninamshukuru Mungu na ninaendelea kujifunza, kusoma vitabu na kufanya mazoezi na niko tayari kuendelea kutoa mchango wangu wa hali na mali ndani na nje ya chama,” alisema.

Desemba 13, mwaka jana, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), iliagiza makada watatu wa chama hicho akiwamo Kinana, waitwe na wahojiwe na Kamati ya Maadili na Usalama, baada ya kutuhumiwa kwa makosa ya kufanya mambo kinyume na taratibu za chama.

Kamati Kuu, iliwaadhibu viongozi hao na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Memba, kufukuzwa uanachama kwa kukiuka maadili ya chama hicho.

Kadhalika, Makamba alisamehewa huku Kinana akipewa barua ya onyo ikiwamo kuwa chini ya uangalizi kwa miezi 18 na kuzuiliwa kujihusisha kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho.