Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tandahimba kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) Selemani Bakari Namkulya Pamoja na Mwenyekiti Chama Cha ACT Wazalendo Juma Halidi Mngawa leo Jumamosi Juni 6, 2020 wametangaza rasmi kujiunga na Chama Cha Mapunduzi (CCM) kutokana na kuvutiwa na maendeleo ambayo Wananchi wamekuwa wakiyahitaji kwa muda mrefu yakitekelezwa na Rais Magufuli hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kubaki huko zaidi ya kurudi kuungana na Rais Magufuli kuleta maendeleo kwa Watu.

"Nikiwa na akili timamu nimeshawishika kujiunga na CCM kutokana na mambo makuu matatu ambayo ni muundo, Sera na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya kuwaletea maendeleo Watu unaofanywa na Rais Magufuli zaidi ya tulivyotarajia. Naungana na Rais Magufuli kuyaendeleza maendeleo anayoyafanya kwa Taifa." Alisema Ndugu Selemani Namkulya aliyekuwa Mwenyekiti Halmashauri na Diwani wa Kata ya Mihambwe iliyopo Tarafa ya Mihambwe.

Kwa upande wake Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu aliwapongeza kwa kurudi nyumbani CCM chama chenye muundo, sera, kanuni na kinachoendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho.

"Mnamo Februari 21, 2020  CCM ilimpokea aliyekuwa Mbunge wa CUF Tandahimba Mhe. Katani Ahmed Katani ambaye ni Mwananchi wangu wa kata ya Kitama; leo hii Juni 6, 2020 CCM imempokea Ndugu Selemani Namkulya aliyekuwa Mwenyekiti Halmashauri na Diwani wa Kata  Mihambwe iliyopo Tarafa ya Mihambwe.

Ni faraja kuona viongozi hawa wakubwa wanaungana na CCM, chama chenye muundo mzuri, sera safi na ilani ya uchaguzi inayooongoza nchi. Karibuni tujumuike pamoja kumuunga mkono Rais Magufuli anayefanya kazi kubwa iliyotukuka ya kuijenga Tanzania mpya na ya mfano bora Duniani kiuongozi na kimaendeleo." Alisema Gavana Shilatu.

Tukio hilo la kukabidhiwa kadi limefanyika ofisi ya CCM wilaya na Mwenyekiti CCM wilaya, akishirikiana na Kamati ya siasa ya wilaya, Sekretarieti wilaya na kushuhudiwa na Afisa Tarafa Mihambwe Gavana Shilatu na Wazee maarufu.