Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja amekipongeza chama hicho kwa kuweka utaratibu mpya wa kupata wagombea ndani ya chama.

Amesema kuwa utaratibu huo unajenga afya ya chama na kufufua matumaini kwa baadhi ya wanachama wagombea walio na sifa lakini siku za nyuma walikata tamaa kutokana na mazingira yake kuwepo mwenye nacho alitumia uwezo wake kupata uongozi hata kama hana sifa ya uongozi lakini ililazimu ashinde tu.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, bw. Khamis Mgeja aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelewa na waandishi wa Habari shambani kwake katika kijiji cha Nyanhembe Kata ya Kilago wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kwa lengo la kujionea shughuli za kilimo na ufugaji anazofanya hivi sasa baada ya kupumzika siasa.

Kada huyo wa chama cha Mapinduzi alisema kuwa uimara wa vyama vyovyote Duniani vilivyo bora na imara hujitathimini vyenyewe na kufanya mabadiliko ndani ya chama na kupelekea kujijenga zaidi na chama cha Mapinduzi CCM kikiwa kimoja wapo Duniani.

Aliendelea kuwaeleza waandishi wa habari hao kuwa kwa mabadiliko haya ya CCM kuhusu kupatikana kwa wagombea na taratibu za vikao vya chama alisema anaimani kuwa CCM inarejesha matumaini kwa baadhi ya wanachama waliokata tamaa kutokana na mizengwe mizengwe ya baadhi ya viongozi huko katika siku za nyuma.

“Nichukue nafasi hii kumpongeza mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli pamoja na sekretaliet inayoongozwa na katibu mkuu wa chama hicho Dkt. Bashiru Ally kwa kukiongoza chama kwa misingi ya haki na mpaka sasa chama kiko imara sana kama kilivyo asisiwa huko nyuma na baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisifu Mgeja.

Aidha Mgeja alisema kuwa kwa uongozi huu wa chama chini ya mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Magufuli na katibu wake mkuu Dkt. Bashiru Ally muonekano wa chama ni mpya na uko imara na kutumia fursa hiyo kuwapa hongera zake za dhati kabisa kwa kukifanya chama hicho kuzidi kuwa imara sana na kuongeza kuwa CCM kuendelea kutetea wanyonge pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema kuwa pamoja na yeye kupumzika siasa hataacha kukitetea, kukisema chama kutokana na mafanikio yake kwa wananchi yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano yanayotokana na utekelezwaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.

Kuhusu utaratibu siku za nyuma za kupata wagombea Ubunge uwakilishi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, mwanasiasa mkongwe, Khamis Mgeja alieleza kwamba chaguzi hizo zilitoa mwanya kwa baadhi ya watu kugeuza Chama kuwa Kama gulio la kutafuta Uongozi.

Mgeja ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga anaufurahia utaratibu wa sasa na kusema hata hivo umechelewa ulipaswa ufanywe siku nyingi sana.

Pamoja na mambo mengine Mgeja alieleza  yaliyokuwa yakishuudiwa siku za nyuma kwenye kata na matawi ambako wagombea walipita kwaajili ya kuomba kura za maoni ndani ya chama nadhani utaratibu ulikuwa siyo mzuri na sahihi kupata viongozi bora.

"Mnabaki kupata Viongozi wenye nguvu ya bahasha na saa nyingine tulikuwa hatupati Viongozi siku za nyuma wenye maadili na sifa za Uongozi, tunaupokea utaratibu huu kwa mikono miwili," anasema Mgeja.

Alisema kuwa kila anayekitakia Chama mema ni lazima aunge mkono mabadiliko haya yanayoanza kutelekezwa chini ya uenyekiti wa Dkt. Rais John Magufuli.

Aliwaambia waandishi wa Habari kuwa anaamini kuwa chini ya utaratibu huu utakomesha mianya ya kununua wapiga kura za maoni ndani ya chama, kitakuwa na fursa ya kuchambua kiongozi mwenye sifa na kutokomeza zama za wanunuzi wa kura.

Mwana siasa huyo mkongwe ameweka bayana yaliyojitokeza siku za nyuma chini ya utaratibu wa zamani wa kura za maoni alisema ilikuwa rahisi kwa mgombea kujiongezea wapiga kura wasio na sifa ya kupiga kura ili lazima ashinde hata kama hana sifa ya kuwa kiongozi.

"Unakuta mwanachama kaweka mikakati michafu ya kutengeneza wanachama waliowaokotwa mitaani wanawakatia kadi na kwenda kuwapigia kura za maoni ili washinde uchaguzi," alisema.

“Kulikuwa na mambo ya hovyo ya kupata viongozi, mtu anakuja na kikundi cha familia yake na kuokota wapiga kura mitaani na kuwagawia kadi. Tunapata viongozi wanaoibuka kama magugu maji  na ndiyo maana siku za nyuma ilitupa shida kujua kiongozi ni nani kama ilivyoainisha baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya vigezo vya kiongozi mzuri,” alilalamika Mgeja.

Alisema kuwa walipishana usiku wa manane kwa wapiga kura, majumbani mwao ili kuwahamasisha, wawapigie kura wananywesha pombe, pilau jambo ambalo siku za nyuma tuliishia kupata viongozi wabovu na wasiokuwa na sifa za uongozi.
 
Mgeja alisema kuwa kama kweli mtu anakubalika hana sababu ya kutumia nguvu kubwa sana bali kiongozi mzuri ni aliyewekeza hisa za imani na uadilifu kwa umma.

Alikumbusha kuwa kipindi kilichopita, uchaguzi uliacha mpasuko na chuki baada ya watu wenye nguvu ya fedha kuteka wanachama ili kujipatia uongozi licha ya baadhi kutokuwa na sifa inayostahili.

Mstaafu huyo wa siasa Mgeja alitumia nafasi hiyo ya kuzungumza na vyombo vya Habari vilivyotembelea shambani kwake huko kijijini cha Nyanhembe na kumuomba maoni yake kuhusu mabadiliko ya taratibu za chama kupata wagombea aliwashauri wanachama wenzake kubadilika na kuacha mazoea katika kutafuta viongozi.

Huku akisema kuwa kila zama na kitabu chake huko siku za nyuma kile kilikuwa kitabu kingine na hivi sasa hiki ni kitabu kingine.

“Nampongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kukirudisha chama katika misingi yake ya asili, matamanio ya wengi ni kuona chama kinapata viongozi wenye sifa, hili wanachama wengi hatuna shaka nalo kwani uongozi wa chama uko imara na makini,” alisema Mgeja.

Mgeja aliongeza kuwa chama kinaposimamia maadili na haki na hasa kipindi cha uchaguzi wa kuwapata wagombea waUbunge na Udiwani wanaotokana na matakwa ya wana CCM na umma wa Watanzania ndipo hupelekea chama kukiacha salama na wamoja.

Mwisho.