Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

USHAHIDI wa awali wa Jeshi la Polisi nchini kuhusu madai ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe umeonesh kuwa siku hiyo ya tukio Mbowe alikuwa amelewa chakali na alizunguka kwenye kumbi mbalimbali za starehe zinazouza vileo ikiwemo ya Royal Village.

Pia ushahidi huo unaonesha mbali ya kuwa kwenye maeneo hayo ya starehe alikuwa nyumbani kwa mzazi mwenzake Joyce Nkya ambaye ni Mbunge wa Viti Maaluma Chadema na kwamba hata taarifa za kwamba ameshambuliwa zinatia shaka kwani mashahidi wote ambao wameojiwa hakuna anayethibitisha uwepo wa tukio hilo zaidi ya Mbowe mwenyewe na dereva wake.

Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi hilo David Misime amesema Juni 9 mwaka huu walitoa taarifa ya awali kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Mroto kuhusu tukio la lililoripotiwa kuwa Mbowe amelezwa jijini Dodoma kwa kile kilichodaiwa kushambuliwa wakati anaingia nyumbani kwake .

Misime amesema baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo ya awali wamekuwa wakipokea simu nyingi kutoka kwa waandishi wa habari wakitaka kufahamu matokeo ya uchunguzi kuhusu taarifa iliyofikishwa Kituo cha Polisi Kati Dodoma.

"Napenda kujulisha kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kufanya upelelezi wa kina kuanzia kwa mhanga mwenyewe wa tukio ambaye alidai kuwa muda wa saa saba hivi usiku akiwa kwenye ngazi ya kuingia nyumbani kwake akiwa na anatoka kwa mzazi mwenzake aitwaye Joyce Nkya ambaye ni Mbunge wa Viti Maaluma Chadema anayeishi eneo la Medeli Mjini Ddoma alishambuliwa na kuumia kwenye mguu wa kulia.

"Mhanga wa tukio hilo alidai wakati anashambuliwa alipiga kelele nyingi kuomba msaada ambao aliupata kutoka kwa dereva wake ambaye naye alipiga simu kwa Joyce Nkya kisha hospitali iliyoko takribani umbali wa kilometa tano nje ya Jiji la Dodoma pasipo umuhimu wa kutoa taarifa Polisi kabla ya kwenda kwa Joyce Nkya na Hospitali,"amesema Misime.

Ameongeza upelelezi wao umepata ushahidi kutoka kwenye eneo la tukio unaonesha kulikuwa na watu kwa namna yoyote wangeweza kusikia makelele yaliyopigwa na Mbowe kuomba msaada na wengine walikuwa na uwezo wa kuona bila kizuizi kitendo cha kushambuliwa .

"Hata hivyo kwa mujibu wa wa mashahidi hawa hakuna hata mmoja aliyeweza kusikia kelele hizo au kuona mbowe akishambuliwa. Kwa mantikini hiyo ushahidi pekee unaozumngumzia kushambuliwa ni maelezo ya mhanga wa tukio(Mbowe) pamoja na dereva wake.

"Ambayo kwa hali ilivyo sasa yanatia shaka kuhusu ukweli wa tukio hili.Mashaka hayo yanaongezeka zaidi pale tulipobaini kuwa nyumbani kwa Mbowe alikuwepo kijana wake aitwaje James Mbowe ambaye hawakuona umuhimu wa kumjulisha kuhusu tukio lililotokea hapo nyumbani badala yake waliona umuhimu wa kumjulisha Jocye Nkya aliyekuwa mbali na eneo la tukio,"amesema.

Pia amesema uchunguzi wa Jeshi la Polisi nchini umethibitisha kuwa siku ya Juni 8 mwaka huu Mbowe alitembelea sehemu kadhaa za starehe zinazouza vileo ikiwepo ya Royal Village na kupata kinywaji.

"Hata hivyo alipofika hospitali alioneana akiwa katika hali ya ulevi chakari kiasi cha kushindwa kutamka maneno sawa sawa.Tunaendelea na uchunguzi kutafuta ukweli wa tukio hili, hivyo tunaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia upelelezi huo wazilete kwetu. Tutaendelea kutoa taarifa kwenu kadri ushahidi utakavyopatikana,"amesema Misime kupitia taarifa ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari.