HOTUBA YA MHE MCHUNGAJI PETER SIMON MSIGWA, AKITANGAZA NIA YA KUWANIA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 14 MWEZI JUNI, 2020, MJINI DODOMA

“Nataka kuwa Rais wa Ndoto Yako.”

I. UTANGULIZI

Waheshimiwa Wananchi Wenzangu wa Tanzania na marafiki wa nchi yetu;
Tarehe 25 Mwezi Oktoba Mwaka huu (2020) tunakwenda kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani wa kuiongoza nchi yetu kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa kawaida, uchaguzi ni kipindi kinachompa kila mwananchi fursa na wajibu wa kuhakikisha tunapata sera na uongozi bora, kwa ama kujitokeza kuwania nafasi ya uongozi au kupiga kura ya kumchagua mtu sahihi wa kuliongoza vema Taifa letu.

Ndugu Wananchi, kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Mimi Mchungaji Peter Simon Msigwa, nimeamua kuchukua wajibu wa kujitokeza ili kuipa nchi yetu fursa pana zaidi ya kupata Rais bora ambaye hajawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.

Kama nilivyokwisha dokeza siku chache zilizopita, leo natangaza rasmi nia yangu ya kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na tayari, kwa mujibu wa Katiba na taratibu za chama chetu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) - nimewasilisha taarifa rasmi ya kuomba kuteuliwa na chama chetu kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

II. KWANINI NAUTAKA URAIS WA TANZANIA

Ndugu Wananchi, nimesukumwa na jambo moja la msingi kutaka kuwania nafasi hii ya juu kabisa ya uongozi wa Taifa letu. Nataka kuongoza mageuzi makubwa ya kiutawala, kiuchumi na kielimu yatakayoleta maendeleo makubwa na ya haraka, yaliyo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya sasa na yajayo ya Tanzania yetu.

Ndugu Wananchi, Viongozi makini huota. Viongozi bora hubeba maono ya aina ya nchi wanayokusudia kuijenga. Ndoto yangu ni kuitoa Tanzania katika orodha ya nchi maskini sana duniani na kuipa mwelekeo sahihi wa kifikra, kiutawala na kisera utakaoiwezesha kuja kuwa miongoni mwa nchi zenye maendeleo makubwa kabisa duniani. Ninayo dhamira ya kweli, maono sahihi na uwezo wa kutosha wa kuiongoza vema Tanzania ili kuifikia ndoto hii kubwa. Naam, ndoto ya Tanzania yenye maendeleo ya uhakika!

Ndugu Wananchi, upo ubishani mkubwa kuhusu hali ya maendeleo ya nchi yetu. Mara zote, wenzetu wa CCM wamekuwa wakitamba kuwa wamefanya mambo mengi sana tangu tupate uhuru na kwamba nchi yetu imeendelea kwa kasi sana! Sote tumesikia jinsi ambavyo Taifa limekuwa likiaminishwa kuwa “tuko vizuri” licha ya kuwa hali ni tofauti sana na vile inavyosemwa.

Ndugu Wananchi, tunapokwenda kuchagua viongozi wapya wa kuongoza nchi yetu, ni muhimu tukamaliza ubishi uliopo kuhusu maendeleo yetu. Ni lazima kila Mtanzania akaelewa vizuri maendeleo ni kitu gani hasa ili sote tukaweze kuchagua watu wanaoweza kutuletea “maendeleo ya kweli” katika nchi yetu. Kwa tambo na imani potofu zinazojengwa na viongozi wa CCM kwamba “eti nchi yetu imeendelea”, nalazimika kutoa tafsiri na tathmini sahihi kuhusu kukwama kwa maendeleo ya nchi yetu.

III. KUKWAMA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU

Ndugu Wananchi, naomba kila Mtanzania anielewe vizuri. Hoja yangu si kwamba hakuna kitu hata kimoja kilichofanywa na utawala wa CCM, bali ukweli ni kwamba chini ya serikali zote za CCM, nchi yetu imeendelea kusuasua kimaendeleo kwa muda mrefu, imepoteza mwelekeo na kushindwa kabisa kupiga hatua kubwa na mpya za kimaendeleo.

Ndugu Wananchi, Kimsingi, mambo yote ambayo CCM imekuwa ikiyataja kuwa ndiyo “maendeleo” bado hayalingani hata kidogo na wingi wa raslimali za nchi yetu wala na muda mrefu wa zaidi ya nusu karne ambao CCM imekaa madarakani.

Aidha, mambo mengi kati ya yale yaliyofanyika chini ya CCM, bado hayana hadhi hata kidogo ya kuitwa “maendeleo”. Mengi ni utatuzi tu wa kero na matatizo madogo-madogo na ambayo yamekuwa yakijirudia- rudia tena mara kwa mara.

Ndugu Wananchi, miaka 59 baada ya uhuru, bado nchi yetu ipo pale pale pa siku zote. Bado Tanzania ni moja ya nchi masikini kabisa duniani.Uchambuzi wa Benki ya Dunia kuhusu Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya (Household Budget Survey) wa mwaka 2018, unathibitisha kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania bado wanaishi katika umaskini wa kipato cha chini ya Dola 1.90 kwa mtu kwa siku. Kwamba, bado wananchi wengi hawawezi kumudu hata mahitaji ya msingi ya kimaisha ikiwemo chakula, mavazi, malazi na matibabu!

Ndugu Wananchi, ushahidi kuwa nchi yetu ipo nyuma na imekwama sana kimaendeleo ni mwingi sana. Naomba Watanzania wote mfahamu kuwa wakati tunapata uhuru mwaka 1960, Tanzania na Malaysia pamoja na nchi nyingine za Mashariki mwa Bara la Asia, almaarufu kama “East Asian Tigers” kama Korea ya Kusini, Singapore, Thailand, Hong Kong na Indonesia, zilikuwa katika kiwango sawa cha maendeleo na idadi ya watu. Leo, miaka 59 baada ya uhuru, Tanzania imeachwa mbali sana na nchi hizo licha ya kuwa Mwenyezi Mungu ametujalia raslimali nyingi zaidi kuliko nchi hizo.

Ndugu Wananchi, kwa mujibu wa Utafiti wa Gate Institute, mwaka 1961 wakati tunapata uhuru kutoka kwa Mkoloni, Tanzania na Malaysia zilikuwa karibu sawa kwa idadi ya watu na kwa wastani wa Pato la kila mtu (GDP Per Capita). Wastani wa Pato la kila Mtanzania ulikuwa ni Dola za Kimarekani 319 wakati wastani wa Pato la kila raia wa Malaysia ulikuwa ni Dola za Kimarekani 299. Lakini hadi kufikia mwaka 2018, wastani wa Pato la Mtu Tanzania ulikuwa umefikia Dola za Kimarekani 1,090 tu wakati kwa Malaysia Pato la Mtu lilikuwa limefikia Dola za Kimarekani 12,109.

Ndugu Wananchi, hii ni sawa na kusema kuwa Pato la Mtu nchini Malaysia limeongezeka mara 12 zaidi ya Tanzania. Wakati Tanzania inahangaika kufikia hadhi ya nchi zenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, tayari Malaysia imeshafikia hadhi ya juu zaidi ya nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.

Ndugu Wananchi, kupitwa na kuzidiwa na nchi hizi tulizowahi kuwa nazo sawa kimaendeleo, hakujatokea kwa bahati mbaya! Wala umasikini wetu wa vipato, ukosefu wa ajira, upatikanaji mgumu wa huduma za afya, maji, kilimo duni na mengineyo mengi yasiyoridhisha na yanayokatisha tamaa, havijatokea kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya kukosa uongozi bora kutoka CCM.

Ndugu Wananchi, leo CCM haiwezi kubisha hata kidogo kwamba haikwenda kujifunza uongozi bora wala kuiga mikakati ya maendeleo kutoka Malaysia. Na wala hawawezi kubisha hata kidogo kwamba ule Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa “Big Results Now” uliandaliwa kwa kuiga Malaysia. Siyo kosa kuiga! Tatizo ni kwamba wameshindwa kabisa kutekeleza hata kile walichogelezea kutoka Malaysia!

IV. UCHUMI WA ASILIMIA 7 USIOPUNGUZA UMASKINI

Ndugu Wananchi, Serikali ya “Hapa Kazi Tu” nayo imeendelea kujivunia ukuaji uchumi ule ule wa asilimia 7 ambao umekuwapo kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita. Yaani tangu wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa! Hakuna jipya tena lililoongezeka katika uchumi wetu wala katika ustawi wa jamii zetu.

Ndugu Wananchi, miaka 59 baada ya uhuru, bado wanawake wengi wajawazito na watoto wanapoteza maisha kila siku kwasababu ya huduma duni za afya. Bado wananchi wengi wa vijijini wanatembea umbali mrefu kutafuta maji ya kunywa na ya kutumia majumbani mwao. Bado maelfu ya vijana wa Kitanzania hawana ajira wala matumaini ya kuwawezesha kumudu maisha yao.

Ndugu Wananchi, tafiti zinathibitisha pasipo shaka kuwa ukuaji uchumi wa asilimia 7 ambao serikali imekuwa ikijivunia bado haujaweza kuwapunguzia wananchi umasikini. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Shirika la ESRF kuhusu Ukuaji Uchumi Usiopunguza Umaskini – yaani “Growth without Poverty Reduction in Tanzania, uchumi wetu umekuzwa zaidi na sekta za ujenzi, huduma na madini ambazo hazijaajiri Watanzania wengi. Sekta ya kilimo inayoajiri Watanzania wengi haijapewa kipaumbele inachostahili.

Ndugu wananchi, Serikali ya Awamu ya Tano ni mfano mbaya zaidi wa namna serikali za CCM zinavyopuuza kilimo. Kama tulivyosema juzi Bungeni, wakati kilimo kinaajiri takribani asilimia 80 ya wananchi wote, ndani ya kipindi cha miaka mitano, serikali hii inayomaliza muda wake imetekeleza bajeti ya miradi ya maendeleo ya kilimo kwa asilimia 17.55 tu. Asilimia 82.45 ya bajeti ya miradi yote ya maendeleo haikutekelezwa kabisa katika kipindi cha miaka mitano. Ni dhihaka kubwa kwa Watanzania kwa serikali hii ya Awamu ya Tano kujiita serikali ya wanyonge.

Ndugu Wananchi, tunapokwenda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, naomba kila Mtanzania akumbuke kwamba tayari serikali za CCM zilishabuni sera na mipango mingi ya kimaendeleo lakini yote ilishindwa kuleta maendeleo yaliyokusudiwa. Si Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) wala Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA)! Si Mkakati wa Kilimo Kwanza wala wa Mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa! Si Ahadi za Maisha Bora kwa Kila Mtanzania wala Ahadi ya Tanzania ya Viwanda! Si hekaya za Kasi Mpya, Nguvu Mpya na Ari Mpya wala hadithi za Hapa Kazi Tu! Mikakati na jitihada zote hizo tayari vilishindwa kabisa kuipatia Tanzania yetu maendeleo ya uhakika.

Ndugu Wananchi, kila uliposhindwa Mpango mmoja basi ulianzishwa Mpango mwingine na kutafutiwa kauli mbiu au vibwagizo vya kuwalaghai upya wananchi. Hakuna jipya tena ambalo serikali ya CCM inaweza kufanya katika nchi hii likafanikiwa. Uzoefu wa CCM ni kushindwa. Umahiri wa CCM ni kutoa ahadi hewa na kushindwa kuzitekeleza. Udhaifu wa CCM ni kukosa dira na mwelekeo sahihi wa kushughulikia maendeleo ya nchi yetu. Uwezo wa CCM umeishia kwenye kushughulikia matatizo na kero ndogo-ndogo ambazo hata baada ya kutatuliwa kwake bado hakuifanyi nchi yetu kuwa na maendeleo makubwa.

Ndugu Wananchi, kama walivyosema Wahenga wetu – “La kuvunda, halina ubani” na “Kuvuja kwa Pakacha, nafuu ya Mchukuzi”. Nimeamua kujitokeza kuomba fursa ya kupitishwa na CHADEMA kuwania Urais wa nchi hii ili panapo majaaliwa nikawe “Mchukuzi Wenu”.

V. MWELEKEO SAHIHI WA TANZANIA NINAYOTAKA KUIONGOZA

Ndugu Wananchi, Mchambuzi maarufu wa masuala ya Mawasiliano na Maendeleo, Bi Joscelyn Duffy, aliwahi kusema hivi, ninamnukuu:

“Development is beyond solving-problems. When our work is solely about solving a problem, then doing so often it will not spur us beyond the status quo. It simply returns us to it. By solely solving a problem we are essentially not challenging ourselves to stretch beyond what we already know is possible. Beyond solution lies evolution and revolution...and there is where real development is.”

Ndugu Wananchi, kwa tafsiri ya Kiswahili, Mtaalam huyu alisema hivi:

“Maendeleo ni zaidi ya kutatua matatizo. Pale kazi yetu inapokuwa imejikita tu kwenye kushughulikia matatizo, basi kufanya hivyo hakuwezi kututoa kutoka kwenye hali duni tuliyonayo. Sana sana kunaturudisha pale pale tulipo. Kimsingi, kwa kuegemea tu kwenye utatuzi wa matatizo, tunakuwa hatufanyi mambo mapya na yenye tija kuzidi yale ambayo tunajua yanawezekana. Mbali na kutatua “kero na matatizo” madogo-madogo, bado kuna “mageuzi” na “mapinduzi” yanayopaswa kufanywa ...na hapo ndipo maendeleo yalipo.”

Ndugu Wananchi, miaka 59 baada ya uhuru hatuhitaji tena serikali inayohangaika na kero na matatizo madogo-madogo ya kila siku. Hatuhitaji tena Rais wa kuhesabu matundu ya vyoo yaliyojengwa na serikali yake na kutueleza jinsi tulivyoendelea. Hatuhitaji Rais wa kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa madaraja. Wala hatuhitaji Rais anayetafuta wapi kuna Tawi jipya la Benki nikakate utepe kufanya uzinduzi. Wakati tulionao ni wakati wa kuwa na Rais atakayeiongoza nchi yetu kwenye mambo makubwa na ya msingi zaidi. Tunahitaji Rais wa kufanya mageuzi na mapinduzi makubwa ya kiutawala, kiuchumi na kielimu.

Ndugu Wananchi, nimejiandaa vizuri kuipatia nchi yetu Rais wa namna hiyo. Nasubiria ridhaa ya chama change, nasubiria kura za Watanzania wote. Kwa pamoja, nataka tuifikie ndoto ya kuwa na Tanzania yenye maendeleo makubwa, ya haraka, jumuishi na yaliyo endelevu kwa mustakabali wa sasa na wa baadaye wa Taifa letu. Kila Mtanzania anataka maendeleo. Ndoto hii ni ndoto ya kila Mtanzania. Nataka kuwa Rais wa Ndoto Yako.

Ndugu Wananchi, endapo nitapata heshima, imani na dhamana ya kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali yangu itajikita kutekeleza vipaumbele vikuu vitatu: Mosi, ni kufanya Mageuzi Makubwa ya Kielimu, pili kujenga Utawala Bora na Uwajibikaji na tatu ni kufanya Mageuzi Makubwa ya Uchumi wa Kisasa.

1. MAGEUZI MAKUBWA YA KIELIMU NA KITEKNOLOJIA

Ndugu Wananchi, hatuwezi kufanikiwa katika jambo lolot kuzidi kiwango cha fikra tulichonacho kwenye jambo hilo. We cannot develop beyond the level of thinking we have. Kiwango cha fikra tulizonazo katika uchumi ndicho hicho kitakachotuamulia aina na kiwango cha maendeleo ya uchumi.

Ndugu Wananchi, hakuna njia ya mkato katika kuyafikia maendeleo makubwa na ya kweli ya Taifa letu. Hakuna short-cut. Msingi wa maendeleo ni fikra. Tofauti kuu iliyopo baina yetu na nchi nyingi zilizoendelea duniani si rangi wala fedha bali ni fikra. Taifa lolote lile duniani linalohitaji kupata maendeleo makubwa ni sharti lifikirie kwanza kutanua fikra za watu wake. Katika muktadha huu, kufanya mapinduzi makubwa ya kielimu na kiteknolojia ndiyo kitakuwa kipaumbele cha kwanza na cha msingi cha serikali yangu.

Ndugu Wananchi, nakusudia kuunda serikali itakayoufumua kabisa mfumo wetu wa sasa wa kielimu ili kuanzisha mfumo mpya elimu utakaozalisha wasomi wenye maono, maarifa, ubunifu na ujuzi mahsusi wa kutekeleza malengo na kupata matokeo sahihi ya maendeleo yanayolengwa kufikiwa na watu.

Kwa ufupi nakusudia kuliongoza Taifa letu kuachana na elimu inayopimwa kwa vyeti pekee na kuanzisha mfumo wa elimu utakaofungamanishwa moja kwa moja na shabaha za kimaendeleo tunazolenga kuzifikia katika kila sekta. Mageuzi haya makubwa ya kielimu yatakwenda sambamba na kukuza maarifa na ujuzi wa kiteknolojia kwaajili ya kuongeza ufanisi katika sekta zote zinazohusika na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ndugu Wananchi, dhamira yangu ni kujenga nchi ya wavumbuzi na wabunifu wa mambo ya kimaendeleo. Ni kujenga Taifa linalojitegemea kiteknolojia, Taifa la watu wenye uwezo wa kujiajiri na kujitegemea kifikra, wanaodadisi na kutafuta ufumbuzi wa kitaalam dhidi ya kero, matatizo na kutusaidia kuifikia ndoto kubwa zaidi ya maendeleo ya Taifa letu. Taifa la uchumi wa viwanda utaotokana na uwekezaji mkubwa na wa kimkakati wa mageuzi ya kielimu na kiteknolojia na sio kauli mbiu na matamko. Nataka kujenga Tanzania itakayofikiria kwanza kutengeneza kabla ya kununua na kuagiza.

2. UTAWALA BORA NA UWAJIBIKAJI

Ndugu Wananchi, kukosekana kwa utawala bora na uwajibikaji kumekwamisha kwa kiasi kikubwa jitihada nyingi za kusukuma maendeleo ya nchi. Mathalan, kilimo kinachoajiri Watanzania wengi kimepuuzwa na kuporomoka si kwasababu serikali haina fedha za kutosha, bali kwasababu tu serikali imepuuza na kuacha kutoa zaidi ya asilimia 80 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kilimo. Aidha, bila ridhaa wala idhini ya Bunge, tumeshuhudia serikali ikielekeza fedha nyingi katika ununuzi wa ndege ambazo zingepaswa kuelekezwa katika vipaumbele vingine vya msingi na vya haraka zaidi vya maendeleo.

Ndugu Wananchi, nakusudia kuiongoza nchi yetu katika kufanya mageuzi makubwa ya kikatiba na ambayo, pamoja na mambo mengine, yatahakikisha tunakuwa na Mahakama, Bunge na Taasisi Huru ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa isiyoingiliwa na serikali katika shughuli wala maamuzi yake. Kupitia mchakato wa Katiba Mpya, tutaimarisha mgawanyo mzuri wa

madaraka na kuhakikisha kunakuwa na mifumo imara ya kuwajibishana ndani ya utendaji wa serikali. Nitahakikisha nchi haipelekwi-pelekwi tu na utashi na matakwa binafsi ya Rais wa nchi au ya kiongozi yeyote yule, bali inaongozwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na mifumo imara ya kitaasisi.

Ndugu Wananchi, nakusudia pia kuiongoza nchi katika kufuta sheria zote kandamizi kupitia mchakato shirikishi wa Katiba Mpya na marekebisho ya kisheria. Serikali yangu itarejesha na kuimarisha uhuru wa kutoa maoni, demokrasia na shughuli za vyama vya siasa na asasi za kiraia ili kuongeza uwazi, ufuatiliaji, uadilifu na uwajibikaji wa pamoja katika uendeshaji wa nchi, matumizi ya fedha za umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

3. MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI

Ndugu Wananchi, mfumo wa uchumi unaofuatwa na serikali iliyoko madarakani umepitwa na wakati na hauendani na mahitaji ya dunia ya sasa. Ni mfumo unaodhibitiwa zaidi na serikali na ambao umeua nguvu ya soko katika kuamua mustakabali wa uchumi.

Matokeo ya mfumo wa uchumi uliopo sasa ni Taifa kuingizwa katika mzigo mkubwa wa madeni na kushindwa kutengeneza ajira na fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa watu. Iwapo serikali ya CCM itaachwa iendelee kuendesha uchumi wa nchi kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya kwa miaka yote, nchi itakuwa maskini kupindukia kwa karne nyingi zaidi.

Ndugu Wananchi, nakusudia kuufumua kabisa mfumo wa uchumi uliopo na kuanzisha mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii katika nchi yetu. Huu ni mfumo unaolenga kuleta maendeleo shirikishi na endelevu kwa kila mtu. Ni mfumo unaokusudia kukidhi kiwango cha chini cha ustawi wa kiuchumi kwa kila mwananchi.

Kimsingi, mfumo huu utaleta pamoja faida za mfumo wa ubepari na ujamaa na kuondoa kabisa hasara zake.
Ndugu Wananchi, wakati mfumo wa uchumi wa kibepari umethibitika kuwa sio mzuri kwa kusababisha na kushindwa kuziba pengo katika ya matajiri na masikini, Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii ninaokwenda kuuanzisha utaziba pengo hilo kwa kutoa fursa za kiuchumi kwa kila mwananchi, na wakati huohuo utatoa hifadhi ya jamii katika nyanja za ajira, huduma za afya, elimu na huduma nyingine za jamii chini ya uratibu makini wa serikali yangu.

Ndugu Wananchi, wakati mfumo wa uchumi wa kijamaa umethibitika kuwa sio mzuri kwa kuminya fursa za watu kumiliki mali na kufanya biashara huria au kuua nguvu ya ubunifu na ushindani wa soko, Mfumo wa Soko Jamii unakwenda kuachilia furs azote hizo kwa Watanzania.

Ndugu Wananchi, kupitia serikali yangu, nchi yetu inakwenda kuwa na Soko Huru lenye mfumo huru wa upangaji wa bei, na pia mfumo wa udhibiti ili kuzuia baadhi ya watu au taasisi kuhodhi mwenendo wa soko. Mfumo huu utatoa uhuru kwa kila mtu kumiliki mali binafsi. Serikali yangu itaratibu utekelezaji wa mfumo huu kwa kutoa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na mazingira ya uhakika ya kisheria na shirikishi ya hifadhi ya jamii.

Ndugu Wananchi, kupitia mfumo huu, serikali yangu itaimarisha nguvu na uhuru wa sekta binafsi kwa kuondoa vikwazo vyote vya kikodi na kibiashara. Ninakwenda kuongoza serikali

itakayotumia ushawishi wa kimkakati wa diplomasia ya kiuchumi kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuanzisha viwanda na biashara za kutosha.

Nitaongoza urasimishaji mkubwa wa raslimali na biashara zisizo rasmi ili zijumuishwe na kunufaika na mfumo rasmi wa kiuchumi na wakati huo huo kutanua wigo wa mapato ya kodi ya serikali kwaajili ya kuchochea zaidi maendeleo ya nchi.
Ndugu Wananchi, Mfumo wa Soko Jamii ndiyo jibu la kufufua na kuimarisha ukuaji wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi inayoajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.

Kwa miaka mingi sekta ya kilimo imeporomoka sio tu kwasababu ya serikali kutofanya uwekezaji makini wa kuwezesha wakulima, bali kwa kushindwa kuvutia uwekezaji na masoko. Kilimo kimekuwa hakilipi si kwasababu ya kukosekana zana bora na za kisasa za kulimia bali kwasababu ya kukosekana masoko ya uhakika. Mfumo huu mpya unakwenda kuongeza mnyororo wa thamani za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuvutia ushindani wa masoko mengi kwaajili ya mazao hayo.

Ndugu Wananchi, kupitia Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii, ninao uhakika kwamba mamilioni ya vijana na Watanzania wote kwa ujumla watakwenda kupata ajira nyingi na za uhakika kupitia shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi zitakazoanzishwa na sekta binafsi iliyo huru na inayosimamiwa vyema.

Ndugu Watanzania Wenzangu na Marafiki wa Nchi yetu, yapo mengi yatakayofanywa na serikali yangu pindi nikipewa ridhaa ya kugombea na chama changu na pindi nikichaguliwa kwa kura nyingi kuongoza nchi yetu. Napenda kusisitiza tena kuwa uchaguzi huu umewapa fursa ya kumpata Rais bora ambaye hajawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.

Ndugu Wananchi, nachukua fursa hii kuwasihi kuwa nyote mjitokeze kwa wingi katika kusikiliza kwa kina maono, sera na ilani za vyama na wagombea. Pimeni sawasawa bila kuweka ushabiki. Enendeni mkachague yaliyo bora kwa mustakabali mwema wa Taifa letu bila kujali ushabiki mlionao kwa vyama vyenu.

Ndugu Wananchi, Uchaguzi ni maisha. Uchaguzi ni suala linalomhusu kila mtu. Kila mtu ahakikishe anapiga kura na anachagua sawasawa. Mwanafalsafa wa Kigiriki, Plato, aliwahi kusema hivi, namnukuu:

“Napenda kuwaambia wale wanaodhani siasa haiwahusu kwamba moja ya madhara ya kukataa kujihusisha na siasa ni kwamba utaongozwa hata na watu uliowazidi akili. Na kwa upungufu wao wa akili watafanya maamuzi ya kila kitu kinachohusu maisha yako”, Mwisho wa nukuu.

Ndugu Wananchi, nachukua fursa hii kuwakumbusha na kuwasihi sana ...kwamba mjitokeze kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Tarehe 25 Oktoba 2020. Tusiache mwanya wa kuongozwa na watu wasiotufaa.

Ndugu Wananchi, kama alivyosema Mwanafalsafa Enstein, “Problems cannot be solved by the same level of thinking that created them”. Matatizo mengi tuliyonayo kama Taifa tangu

tupate uhuru, hayawezi tena kutatuliwa na kiwango kile kile cha akili ndogo kilichotumika kuyasababisha. Akili ndogo, haiwezi kutawala akili kubwa.

Tanzania inastahili kilicho bora zaidi.
Mageuzi Makubwa yanakuja sasa! Nataka kuwa Rais bora wa Tanzania yetu! Nataka kuwa Rais wa Ndoto Yako!
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

Ahsanteni kwa Kunisikiliza.

..........................................
Mchungaji Peter Simon Msigwa
Oktoba 25, 2020,
Dodoma, Tanzania