Afisa habari wa Simba Haji Manara amesema kuelekea mchezo wa Ligi kuu soka Tanzania bara leo Juni 20, 2020, kati ya Simba dhidi ya Mwadui FC, hawatarajii kama kutakuwa na matokeo matatu.


Haji Manara(katikati) akiwa uwanjani katika moja ya mechi za Simba

Kupitia taarifa aliyotuma kwa vyombo vya Habari, amesema wanachojua wao ni ushindi tu hivyo Mwadui watawasamehe kwa hilo.

''Mwadui tunawaheshimu sana walitufunga mechi ya kwanza na pia tuliwafunga kwa taabu sana kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la shirikisho, lakini ni lazima wajue pointi tatu tunazihitaji hivyo tupo tayari kwa hilo'', amesema Manara.

Aidha Manara amesema mchezo utapigwa Saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa taifa, tofauti na ambavyo imekuwa ikielezwa kuwa utapigwa Saa 11:00 jioni.

Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 72 katika mechi 29, wakati Mwadui FC ina pointi 34 katika mechi 29 ikiwa katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.