KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael leo ameondoka Bongo kuelekea Shinyanga kuungana na timu  kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC utakaopigwa Juni 13.

Eymael ameongozana na mtupiaji  namba moja wa timu David Molinga ambaye ana mabao nane kati ya 31 yaliyofungwa na Klabu hiyo pamoja na Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz.

Eymael alirejea Bongo juzi akitokea Ubelgiji alikokuwa kwa ajili ya mapumziko ya lazima yaliyotokana na janga la Virusi vya Corona. 

Molinga alisema kuwa aliachwa Kwenye msafara wa kwanza kwa kuwa hakuwa kwenye orodha ya wachezaji waliotakiwa kusafiri na timu ambayo ilisepa na basi juzi.

Jambo hilo lilipingwa na Ofisa Habari wà Yanga, Hassan Bumbuli ambaye alisema kuwa Molinga alibaki kwa sababu zake binafsi.

Yanga jana ilianza mazoezi na leo inatarajiwa kuendelea na mazoezi Uwanja wa Fresho Complex.