OFA zaidi ya nne zilizomiminika kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison hasa zile kutoka Uarabuni, zinaonekana kumchanganya Mghana huyo.

Taarifa zinaeleza, moja ya klabu kubwa nchini Kuwait, iko tayari kumwaga dola 350,000 (zaidi ya dola 806) kupata saini ya Mghana huyo.

Klabu hiyo ya nchini Kuwait, ipo tayari kumpa Morrison mshahara wa dola 7,500 (zaidi ya Sh Mil 17), kwa mwezi.


Imeelezwa Yanga tayari ilimuongezea mkataba, lakini Morrison anaonekana anataka kwenda kucheza nchini Kuwait ingawa ana ofa nyingine zaidi ya nne.Rafiki wa karibu wa Morrison amesema klabu tatu kutoka katika nchi tofauti za Uarabuni zimeonyesha nia ya kumsajili Morrison.

“Walianza Qatar, si unajua alicheza kule. Kipindi kile baada ya kuifunga Simba tu ndio walikuwa wa kwanza kabisa, akawaambia wasubiri.“Baada ya muda wakaja hao wa Kuwait, majina ya hizi timu siwezi kuyakumbuka, ni ya Kiarabu, magumu kidogo.

“Pamoja na hao wa Kuwait, bado kuna timu ya Abu Dhabi nayo imeonyesha nia. Hapa sasa linakuwa ni suala la ofa tu kupishana ukubwa.


“Mfano katika timu hizo, moja inatoa fedha ya usajili si kubwa sana lakini mshahara wao ni mkubwa zaidi ya wale waliotoa fedha ya usajili kubwa,” kilifafanua chanzo hicho na kuongeza.

“Ninavyomuona Morrison bado hakuwa ameamua afanye nini, ukiangalia hapa alikuwa na ofa Yanga ambao aliwapa nafasi ya kwanza lakini pia Simba ambao walikuwa na ofa nzuri sana lakini naona akapata hofu kuwa akisajili huko, hawatamruhusu kuondoka kwenda Uarabuni wakati kwa Yanga inaonekana alipoongeza mkataba, walikubali kipengele kuwa anaweza kuondoka wakati wowote lakini si kujiunga na timu ya Tanzania.

”Pamoja na kutakiwa na klabu kutoka katika nchi tatu za Uarabuni, Morrison pia alikuwa amefanya mazungumzo na timu mbili za Afrika Kusini, moja ikiwa ni klabu yake ya zamani ya Orlando Pirates.

Tangu ametua nchini, Morrison amekuwa gumzo kubwa kutokana na uwezo aliouonyesha mara tu baada ya Yanga kumsainisha mkataba mfupi wa miezi sita ambao ulikuwa unampa ruhusa ya kufanya mazungumzo na klabu nyingine.

Mkali huyo kutoka Ghana ambaye aliwahi pia kuichezea AS Vita ya DR Congo, umaarufu wake ulizidi kupanda baada ya kuitungua Simba bao pekee lililoipa Yanga ushindi wa 1-0 katika mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara, msimu huu iliyochezwa Machi 8.