China imeionya Marekani kuwa italipiza kisasi baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza vikwazo dhidi ya wanafunzi wa China nchini Marekani katika hatua ya kulalamikia sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hong Kong. 

Trump alisema Ijumaa kuwa Marekani itawapiga marufuku baadhi ya wanafunzi wa China katika vyuo vikuu na kuanza kupitia upya hadhi maalum ya Hong Kong katika forodha na masuala mengine, wakati China ikiendelea na mpango wa kutekeleza sheria hiyo . 

Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya China, Zhao Lijian amesema maneno yoyote na hatua za kuathiri maslahi ya China zitakabiliwa na hatua za kulipiza kisasi kutoka upande wa China.

 Bunge la China Alhamisi iliyopita liliidhinisha mipango ya sheria hiyo, ambayo itaadhibu vitendo vya harakati za kutaka kujitenga, kuhujumu nguvu za dola, ugaidi na vitendo vinavyohatarisha usalama wa taifa pamoja na kuyaruhusu mashirika ya usalama ya China kuhudumu waziwazi mjini Hong Kong.