Msemaji wa Jeshi la China ametoa onyo kali kwa India kuhusu vitendo vyake vya kichokozi katika eneo la mpaka wa nchi hizo mbili.

Msemaji wa Jeshi la China, Kanali Zhang Shuili katika eneo la kivita la magharibi mwa nchi hiyo, leo Jumatano ametoa tamko rasmi kuhusu mapigano yaliyotokea baina ya China na India katika mpaka wa nchi hizo mbili huko Ladakh na kuitaka New Delhi iache kufanya vitendo vya kichochezi.

Kanali Shuili amesema, bonde la Galwan daima limekuwa ni mali ya China na kwamba wanajeshi wa India wamekanyaga vibaya makubaliano ya mpakani baina ya pande hizo mbili ambayo yalifikiwa katika mazungumzo baina ya makamanda wa kijeshi wa nchi hizo mbili. Amesema, kitendo hicho cha jeshi la India kimetoa pigo kubwa kwa uhusiano wa nchi hizo mbili.


Msemaji huyo wa eneo la vitani la magharibi mwa China pia ameitaka India ifanye haraka kurejea kwenye njia sahihi ya kutatua masuala yanayojitokeza kwa njia ya mazungumzo si kupitia chokochoko za kijeshi.

Wakuu wa kijeshi wa India jana usiku walidai kuwa wanajeshi 20 wa nchi hiyo wameuliwa na wanajeshi wa China katika mapigano yaliyozuka kwenye bonde la Galwan katika eneo la Ladakh la mpaka wa nchi hizo mbili. 


-Parstoday