Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe anaendelea kupata uangalizi wa ziada chini ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Aga Khan, baada ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya ziada tangu alipofikishwa hospitalini hapo.

 
Taarifa hiyo ya chama imetolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene na kusema kuwa uangalizi huo unahusisha saa 72 za kupumzika baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia na uchunguzi wa ziada wa maeneo mengine ya mwili, uliofanyika siku ya Jumatano ambao bado unaendelea.

"Wakati tukiendelea kumtakia kila la heri Mwenyekiti Mbowe baada ya upasuaji huo ambao ni wa kwanza tangu aliposhambuliwa na kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake, pamoja na kwamba hatuna uhakika atalazimika kufanyiwa upasuaji mara ngapi au uchunguzi na matibabu ya ziada yatachukua muda gani na yatabaini nini, tunayo matumaini kuwa Mwenyezi Mungu atamsaidia kupona kwa haraka na kumrudisha katika siha njema" imeeleza taarifa hiyo.

Mbowe amekuwa katika Hospitali ya Aga Khan tangu Juni 9, 2020, alipofikishwa na kupokelewa kitengo cha dharura akitokea Dodoma baada ya kuvamiwa, kushambuliwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana alipokuwa akielekea nyumbani kwake.