Na Amiri Kilagalila,Njombe 

Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema mkoa wa Njombe kimesema kinaamini ushindi mkubwa katika maeneo mengi ya mkoa wa Njombe kwa kuwa wamejipanga kikamilifu licha ya mitiani yote wanayopitia. 

Hayo yamebainishwa na viongozi wa chama hicho mkoani Njombe wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza madiwani wanaotokana na chama hicho wa halmashauri ya mji wa Makambako kwa kuvumilia na kufanikiwa kumaliza kipindi chao cha miaka mitano. 

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe Rose Mayemba amesema ili kuendelea kulinda heshima ya chama na wananchi walio wachagua na kuwaamini madiwani hao,kilichobaki ni kwenda kupambana ili kuonyesha nguvu zaidi na kuijenga halmashauri. 

“Niwatakie mshikamano ili tukafanye zaidi ya hapa tulipofanya na ninaamini Chadema Makambako mnakwenda kushinda halmashauri kwa ghalama yoyote na mkishinda tutarudi kwa ndugu yetu wa Simanjiro aondoke kwenye mkoa wetu kwasababu ubashiri wake utakuwa haujafanya kazi sawa sawa na tunaahidi tutachukuwa na Njombe mjini ” Rose Mayemba mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe 

Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) jimbo la Makambako Lea Meshack Sakalani,licha ya kutoa pongezi zake kwa madiwani wanaotokana na chama hicho kwa uvumilivu wao,ameweka wazi ushindi wa kishindo kwa viti vya madiwani wa halmashauri hiyo licha ya maneno yaliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka kabla ya kikao cha baraza la madiwani kutoa kauli ya kurudisha nyuma juhudi zao.

“Sina cha kuwalipa madiwani hawa waliovumilia,kwa kweli mmetuvisha nguo,najua mmefuatwa vya kutosha lakini mkajua thamani ya Chama ninaomba muendelee kukishika Chama na tutakuwa na ninyi popote na tunaamini mtarudi kwenye nafasi hizo”alisema Lea 

“Yule ambaye alisema kwenye baraza la kuvunja madiwani kwamba kwenye mkoa wa Njombe hafikilii wala hataona kwamba hakuna chama chochote cha upinzani kitakachoshinda kwenye mkoa wa Njombe,nimwambie tu tutatoka na wabunge,tutatoka na madiwani na dhamira yetu sio madiwani tu tunakwenda kuchukuwa halmashauri ya Makambako”aliongeza tena Lea 

Baadhi ya madiwani wa chama hicho waliomaliza miaka mitano akiwemo Ednada Nyagawa diwani wa viti maalum Makambako na mwenyekiti wa madiwani hao,amesema katika baraza la madiwani walifanikiwa kuonyesha uwezo wao wa kusimamia hoja licha ya changamoto walizopitia huku Daud Tweve ambaye ni diwani wa kata ya Makambako na mnadhimu wa madiwani hao ameshukuru chama hicho kwa kumuamini katika kipindi chote cha miaka mitano huku pia akitangaza kwa sasa kuwania nafasi ya urais kutoka mkoa wa Njombe ndani ya chama hicho.