Benard Membe
TAZAMA VIDEO HAPA


Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe amesema, anatamani kujipima ubavu na Rais John Pombe Magufuli katika kinyang’anyiro cha Urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Mwanasiasa huyo ametoka kauli hiyo jana Jumamosi tarehe 20 Juni 2020 akiwa mkoani Lindi ambapo alizungumza na wananchi kuhusu adhima yake ya kuwania Urais wa Tanzania.

Membe amesema, yeye ndiye anayeweza kuufanya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 ukawa na msisimko 'ukanoga' huku akiwataka vijana wenye imani na naye kuendelea kuwa watulivu wakisubiri kuona nini kitaendelea.

Hata hivyo, Membe ameonyesha wasiwasi kama hilo litawezekana kutokana na kile kilichofanywa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kutangaza kumvua uanachama.

Membe amesema, wamefikiria kugombea ndani ya CCM na kufikia,”mwafaka kuwa sisi hatujamkosea mtu, sisi hatujawa waharifu, sisi hatujawa woga na tunajiamini na sisi tunaweza kugombea kabisa kwa sababu tu tunalindwa na katiba na siyo tamaduni.”

“Sisi tunaheshimu uamuzi wa Kamati Kuu, mwenyekiti wake, lakini kamati kuu isime kuwa sisi tulichokifanya ni mapendekezo tu na uamuzi utakwenda kufanya na mkutano wa Halmashauri kuu itakayokutana mwezi ujao wa saba.”

“Kama kamati kuu itasema ilichotamka ni makosa nje ya utaratibu, wakosema alichokisema Membe ni sahihi na shughuli za urais zipo sasa, sasa hivi Membe yuko huru kugombea, kujipima na Rais, wakitamka hivyo, kesho Jumatatu nitajaza fomu ya kugombda urais,” amesema Membe huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wakimsikiliza

“Lakini kama kamati kuu ikibaki na msimamo wake, huwezi kunituma niende Dodoma, nikikataliwa kupewa fomu, nikipewa hiyo fomu nikaenda mikoani na nisipowakuta kuwa wameitwa Dodoma, haitawezekana,” amesema

Akiendelea kuzungumza kwa umakini, Membe amesema,”Kwa hiyo, kugombea kwetu ndani ya CCM, na kuwa na msisimko kama Zanzibar, mnogeshaji ni mimi.”

“Mimi sitakwenda Dodoma mpaka kamati kuu au mjumbe wa kamati kuu, katibu mkuu au katibu mwenzk akinieleza uko huru na tusipofanya hivyo tutaingia kwenye mitego. Kama hatutapata ridhaa tunakitakia kila la kheri chama katika uchaguzi huu,” amesema.

Membe aliwaeleza wananchi hao kuwa,”Uchaguzi ni Oktoba na huu ni mwezi wa sita, chochote kinaweza kutokea hapa katikati.”

Kauli hiyo iliibua shangwe na kuendelea kusema,”Sasa naomba vijana wote kwa jina la Mungu, mtulie, msilete ghasia yoyote, hatujui Mungu alichotupangia, naelewa jinsi mioyo yenu inavyowaka moto.”

“Lengo tuwe na uchaguzi huru na wengine sisi tutaendelea kusema ukweli kwani msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” amesema

Uamuzi wa Membe kuvuliwa uanachama CCM ulitangazwa mbele ya vyombo vya habari tarehe 28 Februari 2020 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kwa kile alichosema, Membe amekuwa hana mwenendo mzuri ndani ya chama hicho tangu mwaka 2014.

Alisema, Membe amekuwa akionyesha mwenendo ambao si mzuri licha ya kupewa adhabu ambazo zililenga kumsaidia ajirekebishe.

Hata hivyo, Dk. Bashiru Ally aliwahi kunukuliwa akisema, hayo ni mapendekezo ya kamati kuu ambayo watayawasilisha katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kwa uamuzi wa mwisho wa kuyaridhia kufukuzwa au kubatirisha.

Dk. Bashiru alisema kikao cha Halmashauri Kuu iliyokutana tarehe 13 Desemba 2019 jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti, Rais Magufuli iliazimia kumwita na kumhoji Membe na wanachama wengine kwa ukiukwaji wa maadili.

Katibu mkuu huyo alisema, uamuzi wa mwisho utafanywa na kiko hicho pindi kitakapokutana.

Wakati uamuzi huo ukisubiriwa na mchakato wa uchukuaji wa fomu za Urais ukianza tarehe 15 hadi 30 Juni 2020, Membe ameibuka akionyesha kutaka kugombea Urais ndani ya chama hicho.