Baadhi ya Nchi za Ulaya zimeanza kutambua na kupongeza hatua ambazo Tanzania imezichukua katika kupambana na Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19 kutokana na muongozo wa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwa zinaendana mazingira na hali halisi ya Tanzania.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bw. Dag-IngeUlstein ametoa pongezi hizo na kutambua jitihada za Rais Dkt John Pombe Magufuli za kutoweka zuio kwa watanzania kutotoka nje (lockdown) kama nchi nyingi duniani zilivyofanya huku tahadhari ikitolewa kwa wananchi kujikinga na kufuata muongozo wa wataalam wa afya jambo ambalo limeifanya Tanzania kutoathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa ni Dhahiri kuwa ugonjwa wa COVID 19 ni ugonjwa mpya ulimwenguni ambao kila nchi imechukua hatua na afua ambazo zinaendana na hali halisi,mazingira ya nchi husika na kupongeza msimamo wa Tanzania na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoa tahadhari kwa wananchi kufuata muongozo wa wataalam wa afya.

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amemshukuru Waziri huyo wa Norway kwa kutambua jitihada za Tanzania katika kupambana na virusi vya corona licha ya baadhi ya nchi kubeza muongozo wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuweka zuio la kutoka nje (lockdown).

Pia ameishukuru Norway kwa kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya kidiplomasia na maendeleo hususani katika kusaidia jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo yake katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bw. Dag-IngeUlstein yamefanyika katika Ofisi za Wizara za Jijini Dodoma kwa lengo la kuimairisha mahusiano baina ya nchi hizo pamoja na kubadilishana uzoefu katika kupamabana na virusi vya corona.