Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis amemshutumu Rais Donald Trump kwa kuleta mgawanyiko na kutumia vibaya mamlaka yake.

James Mattis alikua Waziri wa Kwanza wa ulinzi wa Donald Trump -lakini akajiuzulu mnamo mwaka 2018

Katika maoni aliyotoa jambo ambalo si la kawaida, Bwana Mattis alisema rais ameamua kugawanya watu wa Marekani na pia ameshindwa kuonesha uongozi uliokomaa.

Anasema alikasirishwa na kufadhaishwa sana na jinsi Bwana Trump alivyoshughulikia maandamano ya hivi karibuni.

Bwana Mattis alijiuzulu 2018 baada ya rais kuamua kuondoa majeshi ya Marekani kutoka Syria. Tangu wakati huo amekuwa kimya hadi utawala wa Trump ulipokosolewa vikali katika gazeti la Atlanta Jumatano.

Kama jibu lake kuhusu ukosoaji huo, Bwana Trump alituma mfululizo wa ujumbe kwenye Twitter ambapo alisema Bwana Mattis alisemekana kuwa afisa wa thamani ya juu zaidi duniani.

“Sikupenda mtindo wake wa uongozi au yeye mwenyewe na wengine wengi wanakubaliana na hilo, “Afadhali aliandika!”

“Donald Trump ndio rais wa kwanza kwa maisha yangu ambaye hawaunganishi raia wa Marekani – hata hajifanyi pengine anajitahidi katika hilo,” Bwana Mattis aliandika katika gazeti la The Atlantic. “Badala yake, anajitahidi kutugawanya.”

Aliendelea kusema kuwa : “Tunashuhudia miaka mitatu ya hatua hizi za kukusudiwa. Tunashuhudia matokeo ya miaka mitatu ya uongozi ambao haujakomaa.

Bwana Mattis pia alizungumzia wimbi la hivi sasa la maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi ambako kuchochewa na kifo cha raia Mmarekani mweusi George Floyd aliyekufa mikononi mwa polisi mapema mwezi huu.Mke wa zamani wa George Floyd : 'Gianna sasa hana baba'

Mke wa zamani wa George Floyd : ‘Gianna sasa hana baba’

Maafisa wanne wameshtakiwa kuhusiana na kifo cha Bwana Floyd kilichotokea Minneapolis Mei 25.

“Maandamano haya yanafafanuliwa na dhamira ya maelefu ya watu ambao wanasisitiza kwamba tuishi kulingana na maadili yetu… kama taifa,” Bw. Mattis aliandika. “Hatustahili kutatizwa na wachache ambao ni wavunjaji wa sheria.”

Afisa huyo aliyestaafu – ambaye alijiuzulu Desemba 2018 alikosoa vikali sera ya kigeni ya rais – na pia akashtumu utumiaji wa jeshi kama njia ya kujibu maandamano yanayotokea.

“Sikuwahi kufikiria kwamba jeshi… litaamrishwa kwa chochote kile kitakachotokea kukiuka haki ya kikatiba kwa raia wake wenyewe,” alisema.

“Kufanya wanajeshi kama njia ya kutatua hili, kama ilivyoshuhudiwa Washington DC, kunasababusha mgogoro… kati ya jeshi na raia,” aliongeza.White House inamlinganisha Trump na Churchill katika Vita Kuu ya pili ya dunia

White House inamlinganisha Trump na Churchill katika Vita Kuu ya pili ya dunia

Mapema wiki hii, maandamano ya amani yalitibuliwa kwa vitoza machomu na mabomu ya risasi katika bustani iliyo karibu na Ikulu ya Marekani.

Kisha Bwana Trump alivuka mpaka ili kupiga picha katika kanisa la kihistoria ambalo lilikuwa limeharibiwa kwa kuchomwa moto wakati wa maandamano.

Hatua hiyo ilisababisha ukosoaji mkubwa na wanachama waandamizi wa Democrats na viongozi wa kidini ambao walimshutumu rais kwa kulenga waandamanaji kwa kukusudia ili kupiga picha sehemu hiyo ya kihistoria.

Bwana Mattis pia alikejeli picha hiyo ya ajabu na kumlaumu rais kwa kutumia vibaya mamlaka yake.

Lakini katika ujumbe wa Twitter aliouandika awali, Bwana Trump alihoji ikiwa maandamano hayo yalikuwa ya amani na kusema “watu wamependa alivyofika kwenye eneo hilo la ibada la kihistoria”.

Kifo cha Floyd kimeibua maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mauaji ya polisi yanayowalenga Wamarekani weusi

Wakati huohuo, mashtaka mapya yametangazwa dhidi ya maafisa wote wa polisi waliofutwa kazi kuhusiana na kifo cha George Floyd huko Minneapolis.

Shtaka dhidi ya Derek Chauvin limepelekwa hadi mauaji ya kiwango cha pili, nyaraka za mahakamani zinaonesha.

Maafisa watatu, awali hawakuwa wameshtakiwa, lakini sasa wanakabiliwa na mashtaka ya kusaidia na kuchochea mauaji.

Kifo cha Floyd kimesababisha maandamano makubwa kote nchini Marekani dhidi ya ubaguzi wa rangi na mauaji yanayotekelezwa na polisi dhidi ya raia weusi wa Marekani.

Idadi kubwa ya maandamano katika kipindi cha siku nane zilizopita yamekuwa ya amani lakini wengine wamebadilika na kufanya vurugu huku hatua za kutotoka nje kwa kipindi fulani hasa nyakati za usiku ikichukuliwa katika miji mbalimbali.Mwanasheria Mkuu wa Marekani Keith Ellison akielezea mashtaka

Mwanasheria Mkuu wa Marekani Keith Ellison akielezea mashtaka

Akitangaza mashtaka hayo mapya, mkuu wa sheria Keith Ellison alisema kwamba nia ni haki ipatikane.

Awali, Derek Chauvin alikuwa ameshtakiwa kwa makosa ya mauaji kiwango cha tatu na kiwango cha pili kwa mauaji ya bila kukusudia. Mashtaka hayo yatasalia katika hati ya mashtaka.

Maafisa wengine watatu ni Thomas Lane, J Alexander Kueng na Tou Thao. Wote wanakabiliwa na mashtaka ya kusaidia na kuchochea mauaji kiwango cha pili na kusaidia na kuchochea kosa la mauaji ya bila kukusudia.

Seneta wa Minnesota Amy Klobuchar amesema katika mtandao wa Twitter kwamba mashtaka mapya ni hatua nyengine muhimu iliyopigwa.

Wakili wa familia ya Floyd Benjamin Crump amesema katika taarifa: “Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki inafikiwa na tunafurahi kwamba hatua hii imechukuliwa kabla ya mwili wa George Floyd kuzikwa.”

Lakini baadae aliambia shirika la habari la CNN kwamba familia hiyo inaamini mashtaka dhidi ya Derek Chauvin yanastahili kuwa mauaji ya kiwango cha kwanza na kwamba wamearifiwa kuwa uchunguzi unaendelea na huenda mashtaka hayo yakabadilika hata zaidi.

Je mkuu wa mashtaka alisema nini?

Bwana Ellison alisema hakuwa na shaka yoyote kwamba halitakuwa jambo rahisi kufanikiwa katika kesi hiyo dhidi ya waliokuwa maafisa wa polisi.

“Kushinda kesi hii ni kazi ngumu, Historia inaonesha kwamba kuna changamoto zilizowazi alisema.

Ni afisa mmoja pekee huko Minnesota ambaye amewahi kuhukumiwa kwa mauaji ya raia akiwa kazini.

Bwana Ellison alisema George Floyd alipendwa na familia yake, maisha yake yalikuwa na thamani na kwamba watatafuta haki kwa ajili yao na wataipata.

Aliongeza kuwa kupata haki katika jamii kwa ujumla ni jambo litakalofanyika kwa mwendo wa pole na ni kazi ngumu lakini raia wa Marekani hawana haja ya kusibiri hadi kesi ya Floyd ifikie ukomo wake ili kuanza kazi hiyo.

“Huu ndio wakati tunahitajika kuandika tena sheria za kuwa na jamii yenye haki,” alisema.

Mashtaka hayo yanamaanisha nini?

Mauaji ya kiwango cha kwanza na pili chini ya sheria ya Minnesota yanahitaji ushahidi kwamba mshtakiwa alikusudia kuua. Shitaka la mauaji kiwango cha kwanza katika kesi nyingi kunahitajika ushahidi kuonesha alikusudia kuua na mauaji kiwango cha pili yanahusiana kwa karibu uhalifu uliodhamiriwa.

Shitaka la mauaji kiwango cha tatu kutahitaji ushahidi kwamba mshtakiwa alitaka mwathirika kufa ila tu viitendo vyake vilikuwa hatari mno na vilitekelezwa bila kuzingatia ubinadamu.

Katika mauaji ya kiwango cha pili, mtu akipatikana na hatia anaweza kufungwa hata miaka 40, miaka 15 zaidi ya shtaka ya mauaji kiwango cha tatu.

Kipi kilichotokea?

George Floyd, 46 alifariki baada ya kukamtwa na maafisa wa polisi nje ya duka moja katika mji wa Minneapolis jimbo la Minnesota.

Kanda ya video ya tarehe 25 mwezi Mei inamuonyesha afisa wa polisi mzungu, Derek Chauvin, akiwa amepiga magoti juu ya shingo ya bwana Floyd ambaye amezuiliwa chini barabarani.

Matukio yaliopelekea kifo cha bwana Floyd yalitokeo katika kipindi cha dakika 30.

Ilianza na ripoti kuhusu noti bandia ya $20. Ripoti iliotolewa jioni ya tarehe 25 Mei, wakati bwana Floyd alinunua pakiti ya sigara katika duka la Cup foods.

Baada ya kuamini kwamba noti ya dola 20 aliyoitoa Floyd ilikuwa bandia, mfanyakazi mmoja wa duka hilo aliripoti kwa polisi.

Bwana Floyd alikuwa akiishi katika mji wa Minneapolis kwa miaka kadhaa baada ya kuhama kutoka Houston katika jimbo la Texas.

Alikuwa akifanya kazi kama mlinzi mjini humo, kama mamilioni ya raia wengine wa Marekani, na alikuwa amepoteza kazi yake kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Bwana Floyd alikuwa mteja katika duka la Cup Foods.

”Alikuwa rafiki wa duka hilo, mteja mzuri ambaye hakusababisha tatizo lolote”, mmiliki wa duka hilo Mike Abumayyaleh alizungumza chombo cha habari cha NBC.

Lakini bwana Abumayyaleh hakuweko kazini siku ya tukio hilo. Katika kuripoti kuhusu noti hiyo bandia, mfanyakazi wake kijana alikua anafuata itifaki za kazi.

Baada ya kupiga simu ya 911 mwendo 20.01, mfanyakazi huyo alimtaka Floyd kurudisha sigara hizo, lakini Floyd alikataa kurudisha kulingana na maandishi yaliotolewa na mamlaka.

Mfanyakazi huyo alisema kwamba Floyd alionekana kana kwamba amekunywa pombe na hakuweza kujizuia, yalisema maandishi hayo. Muda mfupi baada ya simu mwendo wa 20.08, Maafisa wawili wa polisi waliwasili.

Bwana Floyd alikuwa ameketi na watu wengine wawili katika gari ambalo lilikuwa limeegeshwa katika kona moja.

Baada ya kulikaribia gari hilo, afisa mmoja wa polisi, Thomas Lane, alitoa bunduki yake na kumuagiza bwana Floyd kuonyoosha mikono yake.

Bwana Chauvin aliwasili katika eneo hilo. Yeye na maafisa wengine walihusika katika jaribio jingine kumuingiza bwana Floyd ndani ya gari.

Wakati wa jaribio hilo, 20.19, bwana Chauvin alimvuta bwana Floyd nje kutoka katika kiti cha abiria na kumuangusha chini , ripoti hiyo ilisema.

Alilala hapo uso wake ukiwa chini bado akiwa amefungwa pingu.

Ni wakati huo ambapo mashahidi walianza kumrekodi bwana Floyd, ambaye alionekana kuwa katika hali ngumu.

Bwana Floyd alizuiliwa na maafisa, huku bwana Chauvin akimwekea goti lake katikati ya kichwa chake na shingo.

‘Siwezi kupumua’, bwana Floyd alisema na kurejelea mara kwa mara, akimlilia mamake na kuomba tafadhali, tafadhali, tafadhali.

Kwa dakika 8 na sekunde 46, bwana Chauvin aliweka goti lake katika shingo ya Bwana Floyd, ilisema ripoti ya mwendesha mashtaka.

The post Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Marekani amshutumu Trump kwa kuwagawanya Wamarekani appeared first on Bongo5.com.