Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani, Timo Werner, amesema katika mahojiano yake kuwa ni bora kwenda kucheza soka nje ya ligi ya Bundesliga kuliko kujiunga na Bayern iwapo ataamua kuondoka Leipzig.
Werner, mchezaji wa safu ya ushambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani, Die Mannachaft, ana mkataba na Leipzig hadi 2023 lakini inaripotiwa anaweza kuondoka kwa kitita cha euro miliono 60 msimu wa kiangazi.
Bayern wanasemekana walimtaka mwaka 2019 lakini makubaliano hayakuafikiwa, wakati Bayern walipoamua kuelekeza nguvu zao kwa winga wa timu ya taifa ya Ujerumani, Leroy Sane, anayesakata kabumbu na klabu ya Manchester City ya England.
Vinara wa ligi ya Premier Liverpool na Chelsea ni miongoni mwa vilabu ambavyo pia vinamnyatia Werner mwenye umri wa miaka 24. Werner ameliambia gazeti la Bild la hapa Ujerumani kwamba uwezekano wa kuhamia katika klabu ya Bundesliga haupo.
“Bayern ni klabu kubwa, hatuhitaji kulizungumzia hilo. Na Hansi Flick amethibitisha msimu huu kwamba ni kocha mzuri kweli kweli. Lakini iwapo uhamisho litajitokeza kuwa suala muhimu, basi afadhali nihamie nje ya nchi badala ya kujiunga na Bayern,” alisema Werner.
“Ni kwamba kuwa na changamoto katika ligi nyingine kungenivutia mimi zaidi kuliko uhamisho ndani ya Bundesliga.” akaongeza.
Werner pia amesema shukran na utambuzi wa kuheshimiana ni kigezo muhimu jambo ambalo halikujitokeza mwaka jana kwa Bayern huku akisema “Siwezi kujibu ni kitu gani kilichoipa msukumo Bayern wakati huo.” Hata hivyo Werner aidha amesema hana nia ya kuipa kisogo timu yake ya RB Leipzig, ambayo imetinga duru ya robo fainali ya kombe la mabingwa barani Ulaya, Champions League, msimu huu wa joto kwa vyovyote vile.
“Nashukuru sana nilichonacho katika klabu ya RB Leipzig na kwa hivyo singeweza kusema kabisa: “Lazima niondoke katika klabu hiyo!” alisema
The post Werner aitolea nje Bayern Munich, adai ni bora kutimka Bundesliga appeared first on Bongo5.com.