Tanzania imeitaka dunia na Jumuiya za Kimataifa kutambua kuwa kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwahimiza Watanzania kusali na kuliombea Taifa kuondokana na maradhi ya COVID 19 kamwe haikuwa kauli ya kupuuza kanuni za kisayansi za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Akitoa salam za Shukrani kwa Mungu na watanzania kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni hitimisho la siku tatu za kumshukuru Mungu  baada ya maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa homa kali ya mapafu COVID 19 kupungua nchini katika Kanisa kuu la Mtakatifu Albano Dayososi ya Dar es salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema licha ya kauli ya Rais kutaka watanzania kusali bado serikali ilisisitiza kufuatwa kwa kanuni za kisayansi za kuepuka maambukizi ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa,kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Ameongeza kuwa hatua ya Tanzania kufunga maabara yake iliyokuwa ikipima virusi vya Corona hapo awali kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubaini kasoro katika maabara kuu,hatua hiyo iliifanya Tanzania kuchukua hatua ya  kujijengea uwezo wake wa ndani na kujenga maabara mpya yenye uwezo wa kuwapima watu wanaodhaniwa kuwa na virusi vya corona maradufu.

Prof. Kabudi amesema kupitia kwa waumini wa Kanisa kuu la Mtakatifu Albano Dayososi ya Dar es salaam,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anashukrani kubwa sana kwa Mwenyezi Mungu na kwa Watanzania wote kwa kuitikia wito wake wa wananchi kuondokana na hofu na badala yake wamlilie Mungu jambo ambalo maombi hayo yamejibiwa kwa kupungua maambukizi licha ya uwepo wa ubashiri juu ya idadi ya watakaoathirika na kufariki dunia kwa maradhi ya COVID 19 kufikia laki moja kwa Tanzania pekee.

Akizungumza wakati wa mahubiri Canon Francis Xavery kwa upande wake amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutofunga nyumba za ibada ikiwemo makanisa na misikiti licha ya mashinikizo kutoka sehemu mbalimbali jambo lilimfanya mwenyezi Mungu kusikia maombi ya watanzania kwa kuwa walimwamini Mungu.

Padri Jacob Kahemele wa Kanisa la Kuu la Mtakatifu Albano Dayosisi ya Dar Es Salaam kwa upande wake amesema kanisa hilo limeungana na waamini nchini kote kuitikia rai ya Mhe. Rais huku akiwataka watanzania kuacha kujipa hofu hususani katika mambo ambayo yanapita upeo wa binadamu na badala yake kila mmoja kwa imani yake kujinyeyekeza mbele ya Mungu ambaye ni suluhisho la mambo yote yanayoonekana na yasiyoonekana.